News
Chonga, Akemea Idara ya Polisi kwa Kukiuka Sheria za Ardhi

Mbunge wa Kilifi kusini Ken Chonga ameikemea Idara ya Polisi kwa kukiuka sheria na kushirikiana na mabwenyenye kuwahangaisha wakaazi kwenye ardhi zao.
Chonga amekariri kwamba kutokana na ulegevu unaoshuhudiwa kwenye idara ya polisi, baadhi ya mabwenyenye wamekuwa wakiendeleza tabia ya kuwatumia polisi vibaya ili kuwanyanyasa wakaazi kuhusu suala la ardhi.
Aidha ameeleza kuchukizwa na hulka hiyo ya kuwafurusha wakaazi kwenye ardhi zao kwa madai ya kuwa wamiliki halali wa ardhi hizo, akisema wengi wa wakaazi wameishi kwenye ardhi hizo tangu jadi.
Wakati huo huo amesema tayari analenga kufanya mazungumzo na wakuu wa idara ya polisi nchini sawa na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro ili kuibuka na suluhu kuhusu suala hilo.
News
Kindiki, ataka makubaliano kati ya serikali kuu na kaunti kutekelezwa

Naibu wa rais Prof. Kithure Kindiki ametaka makubaliano yote kati ya serikali za kaunti na ile ya kitaifa kutekelezwa kabla ya mwezi Disemba mwaka huu wa 2025.
Akizungumza katika makao yake ya Karen jijini Nairobi Jumatatu 23, Juni 2025, kwenye mkutano wa 27 kati ya serikali kuu na zile za kaunti kuhusu bajeti IBEC, Kindiki alisema kumekuwa na makubaliano ambayo yamekuwa hayafuatiliwi ili kutekelezwa.
Kindiki alisema serikali kuu imejitolea kuhakikisha serikali za kaunti zinafanikisha miradi mbalimbali na kuwataka maafisa wa serikali za kaunti na ile ya kitaifa kushirikiana kwa majadiliano.
Wakati huo huo alisisitiza haja ya kutafuta suluhu la matatizo yanayoathiri utendakazi wa serikali za kaunti huku akipuzilia mbali uwepo wa mzozo wowote baina ya serikali kuu na zile za kaunti.
Taarifa ya Janet Mumbi.
News
Spika Teddy, adai wabunge wa kitaifa wanachangia kutimuliwa kwake ofisini

Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire ameibua madai kwamba baadhi ya wabunge wa kitaifa kutoka kaunti ya Kilifi ndio ambao wanaendeleza njama ya kumuondoa kama spika wa bunge hilo.
Kupitia video ambayo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, Spika Mwambire alisema viongozi hao wameshirikiana na baadhi ya Wawakilishi wa wadi wa bunge la kaunti ya Kilifi ili kuhakikisha wanafanikiwa kumbandua mamlakani.
Mwambire alisema viongozi pamoja na gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Maitha Mung’aro wako na njama fiche ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao ilhali hakuna sababu zozote za kimsingi.
Aidha, Mwambire alisema hadi kufikia sasa hajajua sababu kuu ambazo zinasababisha kutaka kumbandua kama Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi.
Vilevile, alisema hatajiuzulu kama spika wa bunge la kaunti ya Kilifi na kuwakosoa wanaomtaka kuomba msamaha bila kumfahamisha makosa yake.
Taarifa ya Janet Mumbi