News
Chama cha DCP chashinikiza wakenya kupinga mswada wa fedha, 2025

Uongozi wa chama cha DCP unashinikiza wakenya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2025 ukidai una vipengee tata vitakavyoongeza mzigo wa ushuru kwa wakenya.
Kulingana na Naibu Kinara wa chama hicho Cleophas Malala, mswada huo hauzingatii hali ya uchumi ya wakenya ambao wanaendelea kukabiliana na gharama ya juu ya maisha.
Malala alitaja baadhi ya vipengee vinavyoibua maswali kama vile kodi mpya ya kuongezwa kwa ushuru wa VAT kwenye bidhaa za kawaida kama vile vyakula.
Akizungumza mjini Mombasa, Malala alishauri wakenya kuwa makini na kushiriki mchakato wa kuchambua mswada huo kikamilifu vile vile kutoa maoni kwa bunge kabla ya kupitishwa na kuwa sheria.
Malala alimlaumu Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga pamoja na Rais William Ruto akidai wamezihadaa familia zilizowapoteza wapendwa wao mwaka jana wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha kwamba zingefidiwa.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mamlaka ya KPA yalalamikia changamoto zinazolemaza shughuli zake.

Licha ya Bandari ya Mombasa kuendelea kurekodi matokeo bora katika utendakazi wake,mamlaka ya bandari nchini (KPA) imebainisha kwamba bado kuna changamoto zinazolemaza shughuli zake.
Akizungumza katika kikao na kamati ya bunge kuhusu ushirikiano wa kikanda, mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kuwa changamoto hizo ni pamoja na idadi kubwa ya mashirika yanayokagua mizigo, vizuizi vya kupima uzito wa magari (weighbridges), na vizuizi vya polisi barabarani katika eneo la Kaskazini (Northern Corridor).
Kulingana na nahodha Ruto hali hiyo bado inaathiri ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na biashara kwa ujumla.
Nahodha Ruto pia alieleza athari za ada zisizo rasmi zinazotozwa na mashirika mbalimbali, pamoja na ushuru wa CESS unaotozwa na serikali za kaunti kwa mizigo ambayo tayari imekaguliwa na kulipiwa bandarini.
Aliongeza kuwa gharama hizo za ziada zinaathiri ushindani wa Kenya kama kitovu cha biashara katika ukanda wa afrika mashariki.
Wakati uo huo, Ruto aliitaka serikali kuharakisha uboreshaji wa mifumo ya usafirishaji kwa kuongeza matumizi ya teknolojia na kuunganisha mifumo ya upimaji wa uzito wa magari kote nchini.
Kwa upande wake, kamati ya bunge kupitia kwa mwenyekiti wake, Bi. Irene Mayaka, iliahidi kwamba kamati hiyo itafuatilia kwa karibu malalamshi yaliyoibuliwa na kuhakikisha kwamba suluhu mwafaka inapatikana.
Taarifa ya mwanahabari wetu.
News
Gachagua, amkosoa Rais Ruto kwa madai ya uongozi duni

Viongozi wa upinzani nchini wakiongozwa na Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua waliendeleza kampeni za Wantam dhidi ya rais William Ruto wakielenga uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.
Wakazingumza wakati wa ziara yao ya kisiasa katika eneo la Pwani, Kalonzo alimkosoa rais Ruto akisema ameshindwa kuongoza taifa hali na kuendelea kuwanyanyasa vijana wa Gen Z kwa kuwateka nyara kiholela.
Kalonzo hata hivyo alidai kwamba serikali ya Kenya kwanza ina malengo fiche dhidi ya Bandari ya Mombasa, akisema kama wapinzani watahakikisha serikali ya rais Ruto ina hudumu kwa muhula moja pekee.
“Rais Ruto alishindwa kuongoza nchi na kuendelea kuwanyanyasa wakenya hasa vijana wa Gen Z kwani tumeshuhudia utekaji nyara wa kiholela na hata bandari ya Mombasa wako na malengo fiche na hiyo”, alisema Kalonzo.
Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na ambaye pia ni Kinara wa Chama cha DCP, amemkosoa rais Ruto na Katibu wa Muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini COTU Francis Atwoli kwa kuwahadawa wakenya na kusambaratisha uchumi wa nchi pamoja na kufuja fedha za hazina ya NSSF huku Atwoli akilinyamazia suala hilo.
“Pesa ya NSSF imechukuliwa na Rais Ruto na kuendelea kujenga barabara na Bomas hiyo ni kinyume na sheria na hatutakubali na yule kiongozi wa kutetea wafanyikazi Atwoli amenyamaza ama wamekula hiyo pesa pamoja”, alisema Gachagua.
Upinzani waendeleza kampeni za Wantam
Hata hivyo viongozi walioandamana na Kalonzo katika ziara hiyo ya kisiasa eneo la Pwani wakiongozwa na Mgombea wa kiti cha ubunge wa eneo bunge la Magarini Furaha Chengo Ngumbao, walisema serikali imesheheni wizi wa mashamba ya wakaazi wa Pwani na kudia kwamba mamlaka yote yako nchini ya wananchi.
Wengine walioandamana na Kalonzo ni pamoja na Naibu Kinara wa DCP Cleophas Malala, Mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako, Seneta wa Kisii Richard Onyonka miongoni mwa viongozi wengine.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi