Bandari ya Mombasa imepokea meli ya kwanza ya aina yake, MV Grande Shanghai, ambayo imetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa inayowezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira.
Meli hiyo ya urefu wa mita 220 inayomilikiwa na kampuni ya Grimaldi Group, inaweza kubeba hadi magari 9,000, na inatumia mfumo wa umeme wa kujielekeza bila msaada wa kuvutwa.
Tofauti na meli nyingi zilizotangulia, Grande Shanghai ni mojawapo ya kizazi kipya cha meli za mizigo zilizojengwa kwa kuzingatia masharti ya kimataifa kuhusu kupunguza utoaji wa gesi chafu.
Ujio wa meli hiyo unajiri wakati ambao KPA imezindua sera yake ya Green Port ya mwaka 2024–2028, unaolenga kupunguza athari za shughuli za bandari kwa mazingira.
Miongoni mwa hatua zinazopangwa ni pamoja na kuweka miundombinu ya umeme kwa ajili ya meli zinazotia nanga, kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, na kuleta vifaa vya kushughulikia mizigo visivyochafua hewa.
MV Grande Shanghai ni meli ya kwanza kati ya kumi ambazo Grimaldi Group inapanga kuzindua, zote zikiwa na uwezo wa kutumia nishati safi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu