News
Anselm: Viongozi wanajukumu la kutimiza ahadi kwa wananchi

Kaimu Spika wa bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselm Mwadime ametoa wito kwa viongozi wa kaunti hiyo kuwajibika vilivyo katika kutetea maslahi ya wakaazi wa kaunti hiyo kama suala la usalama wao ambao umedorora mno.
Mwadime alisema wananchi wa kaunti hiyo wanaendelea kuhangaika na hakuna mikakati ambayo imewekwa na viongozi wa kaunti ili kupatikane mwafaka.
Mwadime alisema usalama wa wenyeji unapaswa kupewa kipaumbele hasa kwa wahudumu wa bodaboda ambao wamekuwa wakiuliwa katika hali tatanisha.
Wakati huo huo Mwadime alisema ni lazima mauaji ya wahudumu hao wa bodaboda yadhibitiwe vilivyo na wahusika wakabiliwe kisheria na kufikia sasa ni takribani visa 8 vya wahudumu hao wa bodaboda ambao wameuwawa katika kipindi cha mwaka mmoja huku pipiki zao zikiibiwa.
Haya yalijiri katika hafla ya mazishi ya Darmian Legha aliyeuawa kinyama na abiria wawili juma lililopita katika eneo la chuo kikuu Cha Taita na kutoweka na pikipiki yake.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.