News
Ni Lazima Tushinde Paris Asema Arteta

Mkufunzi wa kilabu ya Arsenal Mikel Arteta angali na imani kwamba vijana wake watanyuka Psg ugenini na kufuzu kwenye fainali ya kilabu bingwa ulaya wiki ijayo mjini Paris.
Akizungumza baada ya The Gunners kukubali kichapo cha goli 1-0 mechi ya mkondo wa kwanza Arteta amedai kwamba mchezo huo walipoteza kutokana na vitu vichache vya kimbinu kipindi cha kwanza ambapo wapinzani wao waliwalemea kimbinu zaidi.
“Bado mechi haijaisha ni nusu tu,bado dakika zingine 90 mjini Paris na tunaenda kwa ajili ya kuvuna ushindi hakuna lingine,”Asema Arteta
Kwa mujibu wa mwalimu huyo wanahitaji kuwa katika ubora wao kuangusha Psg kwani wako na timu nzuri ila lengo lao linasalia pale pale kushinda na kufuzu kwenye fainali mwezi wa May 31.
“Ni lazima tuonyeshe uwezo wetu tokea dakika ya kwanza kwamba tunahitaji ushindi huo, nitafanyia mabadiliko ya kimbinu kikosi kabla ya kuelekea Paris na tuko tayari kupindua meza kule.”
Timu hiyo ililazwa goli 1-0 na miamba hao wa ufaransa kupitia goli lake Ousmane Dembele na sasa wanahitaji kushinda kwa zaidi ya magoli 2-0 mechi ya mkondo wa pili ugani Parc De Prince siku ya Jumatano wiki ijayo.
News
Aisha Jumwa akosolewa kutokana na matamshi yake

Jopo la ushauri la viongozi na maimamu wa Takaungu wadi ya Mnarani kaunti ya Kilifi limeeleza kusikitishwa na kauli zilizotolewa na Aisha Jumwa kuhusiana na tukio la mauaji na maziko ya kijana mmoja eneo hilo lililomtaja kama Zakariyah Kirao Charo.
Likizungumza na vyombo vya habari, jopo hilo likiongozwa na sheikh Mahadh Ali wa msikiti Maryam limemkosoa Jumwa kwa kile lilichosema ameuhujumu uislamu kutokana na kauli alizotoa kwenye mtandao wake wa kijamii wa tiktok kuhusiana na mazishi ya kijana huyo.
Sheikh Mahadh amesema Jumwa alidai kuwa familia ya marehemu haikuhusishwa ilhali walichukua wajibu wa kuihusisha familia kabla ya hatua zozote kuchukuliwa ila wanafamilia wenyewe hawakuonyesha ushirikiano akieleza kuwa jopo hilo pia liligadhabishwa na kauli za Jumwa kuhusiana na namna mchakato mzima wa mazishi ulivyofanywa.
Akiunga mkono kauli hiyo Ustadh Mohamed Khamis amesema kwenye mkao huo kuwa amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa Jumwa tangia mtafuruku huo ulipoanza akisisitiza haja ya swala hilo kutotumika kwa namna ya kuchochea wanajamii waislamu na wasio kuwa waislamu katika eneo hilo la Takaungu.

Aisha Jumwa /Picha kwa hisani
Ustadh Mohamed pia amekinzana na kauli kuwa marehemu alisilimishwa akiwa na matatizo ya kiakili akisema ni sharti swala hilo lisiingiziwe siasa.
News
Viongozi wa Kilifi Wapinga Uekezaji wa Mradi wa Kawi ya Nuklia

Wizara ya Kawi nchini imefanya kikao cha mazungumzo na uongozi wa kaunti ya Kilifi, pamoja na wabunge na Wasimamizi wa Shirika la NUPEA kuhusu uekezaji wa mradi wa uzalishaji kawi ya Nuklia katika kijiji cha Uyombo wadi ya Matsangoni katika eneo bunge la Kilifi Kazkazini katika kaunti ya Kilifi.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kikao hicho mjini Kilifi, Waziri wa Kawi nchini Opiyo Wandayi amesema japo viongozi wa kaunti ya Kilifi pamoja na wananchi hawajaridhishwa na uekezaji wa mradi huo, mazungumzo kuhusu mradi huo bado yataendelea ili kuibuka na mwafaka kwani utasaidia pakubwa katika uzalishaji kawi.
Kwa upande wake Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro amesema msimamo wa serikali ya kaunti ya Kilifi pamoja na wananchi bado uko pale pale wa kuendelea kupinga uekezaji wa mradi huo wa mabilioni ya pesa, akisema utafiti uliofanywa umebaini kwamba mradi huo unaathari kubwa kwa wananchi.
Hata hivyo Mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya amesema kama viongozi kutoka kaunti ya Kilifi hawako tayari kupokea mradi huo wa uzalishaji kawi ya Nuklia, akisema changamoto nyingi bado hazitatuliwa katika mradi huo ambazo ni athari kwa wananchi.
Kikao hicho hata hivyo kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi, Mbunge wa Kaloleni Paul Katana, Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, Mbunge wa Ganze Kenneth Tungule, Katibu katika Wizara ya masuala ya vijana na michezo nchini Fikirini Jacobs miongoni mwa viongozi wengine.