News
Tahadhari Yatolewa Kuhusu Mvua Kubwa

Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini imetoa tahadhari kwa wakenya kuhusu mvua kubwa itakayonyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kipindi cha siku saba.
Mkurugenzi wa idara ya hali ya hewa nchini, Dkt David Gikungu, amesema mvua hiyo itakayoambatana na ngurumo za radi inatarajiwa wakati wa alasiri na usiku, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kupata mvua chache asubuhi kabla ya hali ya jua kuchomoza kwa muda mfupi.
Idara hiyo imesema viwango vya joto usiku katika maeneo haya vitashuka hadi chini ya nyuzi joto 9, hali inayoweza kuathiri watoto, wazee, na wagonjwa.
Kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia, na Pokot Magharibi pia zimeorodhesha kati ya ya maeneo yanayotarajiwa kupokea mvua nyingi.
Hali kama hiyo inatarajiwa katika kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, Taita Taveta, na sehemu za Tana River, ambako asubuhi kutakuwa na mawingu na mvua nyepesi kabla ya hali ya mvua kubwa kuanza alasiri na kuendelea hadi usiku.
Wakati mvua ikinyesha maeneo mengi ya kaunti za Mombasa, Kilifi, Lamu, Kwale, Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, na Isiolo yametabiriwa kupata joto nyakati za mchana hadi kufikia nyuzi joto 33.
Wataalamu wa hali ya hewa wamewahimiza wananchi kuwa waangalifu na kufuata ushauri wa serikali, hasa wale wanaoishi maeneo yenye historia ya mafuriko, maporomoko ya ardhi, na miundombinu dhaifu.
News
Kadinali Bacciu Atangaza Kutohudhuria Kikao cha Conclave

Kadinali Giovanni Angela Bacciu ametangaza kujiondoa katika kikao cha siri cha kumchagua Papa mpya kilichopangwa na Ofisi ya Vatican kuanza rasmi mwezi Mei 7.
Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia Wakili wak siku ya Jumanne tarehe 29, Kadinali Bacciu amesema ameamua kutii wasia ulioweka wa Hayati Papa Francis ingawa alidumisha kutokuwa na hatia.
“Kwa kuwa moyoni mwangu nina wema wa Kanisa ambalo nimelitumikia na nitaendelea kulitumikia kwa uamunifu na upendo na kuchangia ushirika na utulivu wa Conclave, nimeamua kutii kama nilivyofanya siku zote wakati wa Papa Francis na nitasalia kuamini kwamba sina hatia”, alisema Kadinali Bacciu.
Kadinali Bacciu mwenye umri wa miaka 78 na mzaliwa wa taifa la Italia amegongwa vichwa vya habari kutokana na msimamo wake huku baadhi ya wachanguzi wakisema uamuzi wake umetokana na sintofahamu zilizokuwepo kati yake na Hayati Papa Francis mwaka wa 2020 baada ya kuagizwa na Papa Francis kujiuzulu kwa kupatikana na kashfa ya ufisadi.
News
Mbogo: Kaunti ya Mombasa Imeshindwa Kutatua Mzozo wa Ardhi

Aliyekuwa mbunge wa Kisauni Ali Mbogo ameikosoa serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kushindwa kutatua suala tata la uskwota linalowakumba wakaazi wengi wa kaunti hiyo.
Akizungumza katika eneo la Kisauni katika kaunti ya Mombasa, Mbogo amesema tatizo la uskwota limeendelea kuwa chanzo kikuu cha migogoro ya ardhi na ukosefu wa usalama katika maeneo mengi ya kaunti ya Mombasa huku serikali ya kaunti hiyo ikionekana kulifumbia macho suala hilo.
Mbogo amedai kwamba maelfu ya wakaazi wa Kisauni na Mombasa kwa jumla wanaishi kwa hofu ya kufurushwa katika ardhi zao walizoishi tangu jadi kufuatia ukosefu wa hati miliki.
Wakati huo huo amedokeza kwamba baadhi ya maafisa wa serikali ya kaunti hiyo wanahusishwa na visa vya uporaji wa ardhi za umma kwa kushirikiana na waekezaji jambo ambalo amelitaja kuwa dhulma.