Entertainment
Self Love!!? Mulamwah Ajizawidi Gari la Kifahari Kusherehekea Siku ya Mazazi

Mchekeshaji na mtangazaji wa redio, David Oyando, maarufu kama Mulamwah, ameadhimisha siku ya mazazi kwa kujizawidi gari la kifahari aina ya Mercedes Benz S550.
Msanii huyo anayependwa kwa ucheshi wake wa kipekee unaochambua maisha ya kila siku, alitumia mitandao ya kijamii kuonyesha hadharani zawadi hiyo ya kipekee aliyojipa kwa siku yake ya kuzaliwa.
“Na kwa zawadi yangu ya birthday… kutoka E-Class Benz hadi Mercedes Benz S-550 ya kisasa, injini ya 4.8L V8 Bi-Turbo,” aliandika Mulamwah huku akiwapa mashabiki wake taswira ya gari hilo jeusi kutoka Ujerumani.
Katika mazungumzo ya wazi, mtangazaji alifichua kuwa fedha alizotumia kununua gari hilo hapo awali zilikuwa zimekusudiwa kugharamia harusi yake na mchumba wake wa zamani, Ruth K.
Hata hivyo, baada ya mahusiano yao kuvunjika, aliamua kutumia akiba hiyo kutimiza ndoto yake ya muda mrefu.
“Nilitumia pesa nilizokuwa nimewekeza kwa ajili ya harusi—lakini mambo hayaendi kama vile unapanga—kulinunua,” alikiri, akitoa mwanga kuhusu mabadiliko ya kihemko na kifedha aliyopitia.
Kupitia chapisho lenye tafakari ya kina, Mulamwah alitumia tukio hilo kuwatia moyo mashabiki wake kwa ujumbe wa matumaini:
“Kwa Mungu hakuna lisilowezekana. Kama kawaida, songa taratibu, songa kwa usahihi. Hata kama watu hawakuamini, wewe jiamini daima.”
Aidha, hakusita kuwashukuru mashabiki wake pamoja na washirika wa kibiashara waliomsaidia kufika alipo:
“Kwa mashabiki wangu na brandi zote, asanteni sana kwa kuniamini na kunisukuma kuendelea mbele,” aliongeza kwa shukrani.
Mulamwah amejiimarisha kama jina maarufu katika tasnia ya burudani nchini Kenya kupitia vichekesho vyake vinavyosambaa kwa kasi mitandaoni, ambavyo vimejikita kwenye maisha halisi ya Wakenya, pamoja na kazi yake ya utangazaji redioni.
Mchanganyiko wa ucheshi, uhalisia na msimamo wake thabiti umemjengea msingi wa mashabiki waaminifu, sambamba na nafasi ya kushirikiana na bidhaa mbalimbali zinazomhusudu kibiashara.
Licha ya kupitia vipindi vya misukosuko—ikiwemo kuvunjika kwa mahusiano na vuta nikuvute mitandaoni—Mulamwah amesalia imara katika utengenezaji wa maudhui na kukuza maisha yake binafsi.
Kuanzia uigizaji jukwaani, uendeshaji vipindi redioni hadi usimamizi wa chapa yake mitandaoni, ameendelea kukua kama msanii mwenye vipaji vingi na ushawishi mpana.
Entertainment
Millennials Bongo Tour: AY Kuwasha Moto Nairobi!

Nguli wa Bongo Flava kutoka Tanzania, AY, ametua jijini Nairobi tayari kwa tamasha linalosubiriwa kwa hamu – Millennials Bongo Tour, litakalowasha moto Kilimani, Jumapili hii, tarehe 1 Juni.
AY ambaye hiyo jana ameachia vibao vipya SIMUONI na SI NDO MANAKE akishirisha na Harmonize na Darasa mtawalia, atakuwa sura ya tamasha hilo la kipekee la muziki wa Afrika Mashariki. Atasindikizwa na mwanamuziki mahiri kutoka Burundi, Kidum, pamoja na DJ Redbone wa Nairobi, anayejulikana kwa kuamsha burudani kwenye kila tamasha.
Tamasha hili linaahidi mchanganyiko wa kipekee wa vibao vya kumbukizi na ladha ya kisasa ya Bongo Flava. AY, anayejulikana kwa vibao vilivyotikisa chati kama Zigo, Touch Me Touch Me, na Microphone, amewaahidi mashabiki onyesho lisilosahaulika.
“Inahisi vizuri sana kurejea Nairobi. Nipo tayari kuwapa mashabiki wangu burudani ya kukumbukwa,” alisema AY mara baada ya kuwasili.
Kuongeza ladha ya kipekee, Kidum atapanda jukwaani na vibao vyake vya kuburudisha kama Mapenzi na Haturudi Nyuma, huku DJ Redbone akikoleza utamu kwa mchanganyiko mtamu wa Afrobeat, Bongo Flava, na nyimbo kali za ukanda huu.
Millennials Bongo Tour si tamasha la kawaida—ni sherehe ya kitamaduni inayotambua muziki wa Bongo kama daraja linalounganisha vizazi na mataifa. Toleo hili linatoa heshima kwa magwiji wa muziki wa Afrika Mashariki waliotengeneza historia na ambao wanaendelea kuwapa msukumo wasanii wapya hadi leo.
“Hili si tamasha tu—ni sherehe ya muziki wa Afrika Mashariki na fursa ya kipekee kwa mashabiki kuungana na magwiji waliounda sauti ya kizazi,” alisema mmoja wa waandaaji wa tamasha hilo.
Entertainment
Sikutaka Pesa, Nilitaka Furaha – Bango Likaleta Vyote, Manu Bayaz

Afisa wa polisi ambaye pia ni muimbaji wa muziki wa Bango, Emmanuel Yaa Baya anayejulikana zaidi kwa jina la kisanii Manu Bayaz, amefichua kilichomsukuma kuingia kwenye muziki wa Bango.
Akihojiwa na Coco FM katika kipindi cha Coco Asubuhi, Bayaz alisema kwamba hajaanza muziki kwa ajili ya kutafuta pesa, bali alitaka kujifurahisha tu. Hata hivyo, nyimbo zake zilianza kuvutia watu wengi na kumpatia umaarufu mkubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Bango wengine wakiitisha huduma zake kwenye sherehe zao.
“Hapo awali haikuwa kwa ajili ya pesa. Nilianza kwa kujifurahisha, lakini watu wakaanza kupenda nyimbo zangu,” alisema Bayaz.
Kutokana na mafanikio hayo, Bayaz aliamua kubadili mtazamo na kuanza kuwekeza zaidi kibiashara kwenye muziki huo.
Akiendelea kuelezea safari yake ya muziki, alitaja changamoto kubwa aliyokumbana nayo kuwa ni kudhibiti kundi la wanamuziki, akisisitiza ugumu wa kuwaunganisha watu wenye malezi na mitazamo tofauti katika kundi moja.
“Kwenye bendi, kila mtu ametoka mazingira tofauti, amekuzwa kivyake. Kuwaunganisha watu kama kumi si jambo rahisi, lakini tunajitahidi,” alisema.
Bayaz analikumbuka kwa furaha tukio la malipo yake ya kwanza katika muziki wa Bango.
“Malipo yangu ya kwanza ndiyo experience nayoikumbuka maisha yangu ya mziki. Nililipwa shilingi elfu hamsini za Kenya (KSh 50,000), Mtu wa kwanza kumtaarifu habari hii ni babangu,” alisimulia.
Alieleza pia kuwa mapenzi yake ya muda mrefu kwa muziki wa Rhumba ndiyo yaliyomsukuma kuimba Bango, akieleza kuwa Bango ni aina ya Rhumba yenye ladha ya Pwani.
“Mimi napenda sana Rhumba. Nilivyoanza kuimba nikaona niende kwenye hiyo njia. Bango ni Rhumba tu, ila lina ladha ya Kipwani.”
Bayaz alianza kuimba akiwa na Sumilani Band na baadaye Ministers Band. Hata hivyo, aliachana na Sumilani baada ya kutofautiana kuhusu jina jipya alilopendekeza kwa bendi hiyo.
Bayaz pia alieleza kuwa alinunua vyombo vyake vya muziki kutoka China ili kuimarisha safari yake ya muziki, huku akiendelea kufanya kazi na bendi ya Sumilani kabla ya kuondoka.