News
Kikao Cha Kujadili Jinsi ya Kusafisha Sumu ya Lead Eneo la Owino Uhuru Kimetibuka

Kikao cha kujadili jinsi kijiji cha Owino Uhuru katika eneo bunge la Jomvu kaunti ya Mombasa kitakavyosafishwa sumu ya Lead kimetibuka.
Hii ni baada ya wakaazi hao ambao ni waathiriwa wa sumu hiyo kutaka kikao hicho kilichojumuisha maafisa wa Mamlaka ya mazingira nchini NEMA na Wanaharakati wa kijamii kusitishwa.
Wakaazi hao wamelalaka kwamba kikao hicho kinatekelezwa kinyume cha sheria huku wakilalamikia kunyanyaswa na Mamlaka ya NEMA katika mchakato wa kupata fidia yao.
Wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika la Center for Justice, Governance and Environment Action Phyllis Omido wamesema tangu Mahakama iagize wakaazi hao walipwe fidia ya shilingi bilioni 2 hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha sheria katika Mamlaka ya NEMA Erastus Gitonga amesema zoezi la kusafisha mazingira ya Owino Uhuru litafanywa kwa hatua ikiwemo kufanya vipimo vya mchanga, maji na mimea katika eneo hilo ili kutathmini kiwango cha sumu.
News
Amref, yaikabidhi kaunti ya Kilifi vifaa ya matibabu vya milioni 13.2

Shirika la Afya la AMREF kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Kilifi wawekeza zaidi katika sekta ya afya ili kukabiliana na magonjwa yaliyosaulika.
Shirika hilo limeikabidhi serikali ya kaunti ya Kilifi vifaa vya matibabu vya thamani ya shilingi milioni 13.2 ili kuwawezesha wahudumu wa afya kutathmini magonjwa mbalimbali yaliyosaulika na kuboresha sekta ya afya mashinani.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya la AMREF humu nchini Daktari Ndirangu Wanjuki, amesema vifaa hivyo vitasaidia katika kubaini magonjwa yaliyosaulika kama vile Kichocho na kuwawezesha wahudumu wa afya kuwahuhudumia wagonjwa ipasavyo.
Akizungumza wakati wa halfa ya kupokea vifaa hiyo katika hospitali kuu ya rufaa ya Kilifi, Gavana wa kaunti Kilifi Gedion Mung’aro amesema vifaa hiyo vitasambazwa katika hospitali na zahanati 15 za kaunti hiyo.
Gavana Mung’aro amesema magonjwa kama vile Kichocho na Matende miongoni mwa wagonjwa mengine yatagunduliwa kwa urahisi na kutibiwa kwani mengi husababishwa na viini kwenye maji machafu hasa kandokando ya mito.
News
Wakaazi wa Matano Mane Walalamikia Ubovu wa Barabara

Wakaazi wa maeneo ya Matano Mane katika wadi ya Sokoke kaunti ya Kilifi wameandamana na kufunga barabara ya kutoka Chuo cha ufundi cha Godoma inayopitia shule ya upili ya Vitengeni Baptist hadi Vitengeni Mjini wakilalamikia ubovu wa barabara hiyo.
Wakaazi hao wakiongozwa na Dan Mwangome, wamesema barabara hiyo imesalia kwa muda mrefu bila ya kukarabatiwa hali ambayo inatatiza shughuli za kibiashara na uchukuzi wa umma.
Wakaazi hao sasa wanasema mvua inazoendelea kuonyesha imesababisha shughuli za uchukuzi kukatizwa mara kwa mara huku viongozi wa eneo hilo wakishindwa kuwajibikia majukumu yao.
Wakati huo huo wakaazi hao wamemkosa Wanakandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzembea kuwajibikia majukumu yake ya kujenga barabara hiyo.