National News
Famau: Maeneo ya Mijini Yameathirika Zaidi na Mihadarati

Mwanaharakati wa kupambana na Mihadarati katika ukanda wa Pwani Famau Mohammed Famau amesema maeneo ya mijini yameoathirika zaidi na utumizi wa mihadarati ikilinganishwa na maeneo ya mashinani.
Famau amesema utumizi wa mihadarati umeathiri pakubwa vijana, akieleza kusikitishwa na swala hilo kwani vijana wenye umri mdogo tayari ni waraibu wa mihadarati.
Mwanaharakati huyo amesema kwamba serikali ina wajibu mkubwa wa kuimarisha vita dhidi ya mihadarati kupitia vitengo husika ili kuwanasua vijana wanaopotoka kila uchao kupitia utumizi wa dawa za kulevya.
Wakati huo huo amewarai wazazi kuwa waangalifu na watoto wao kwa kuhakikisha wanafuatilia mienendo yao ili kuwaepusha na utumizi wa Mihadarati, uhalifu na mimba za mapema.
National News
Chonga: Wakenya Wanaosafiri Ughaibuni Kusaka Ajira Hawazingatii Sheria za Leba

Mwenyekiti wa kamati ya Leba katika bunge la kitaifa Ken Chonga amesema baadhi ya wakenya ambao wanasafiri katika mataifa ya miliki za kiarabu kusaka ajira wamekosa kuzingatia sheria za Wizara ya Leba nchini na kuangukia mikononi mwa walaghai.
Chonga amesema ni lazima wakenya hao wachunguze mawakala wanaowasafirisha katika mataifa hayo kama wanatambulika na serikali, ndipo waingie katika mikataba ya uajiri ambayo imezingatia sheria za Leba nchini.
Akizungumza na Wanahabari mjini Kilifi, Chonga ambaye pia ni Mbunge wa Kilifi Kusini amesema ili wakenya waepuke madhila mbalimbali kutoka kwa waajiri wao katika mataifa hayo ni lazima wasafirishwe na mawakala waliosajiliwa na serikali.
Wakati huo huo amesema japo serikali iko mbioni kuhakikisha inawatafutia wakenya kazi katika mataifa ya ughaibuni ni lazima wanaosaka ajira za ughaibuni waingie katika mkataba wa uajiri kabla ya kusafiri nje ya nchi.
National News
Chibule: Visa vya Dhulma za Kijinsi Vimepungua Kilifi

Serikali ya kaunti ya Kilifi imesema visa vya dhulma za kijinsia katika kaunti hiyo vimepungua kwa kiwango kikubwa.
Kulingana na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Flora Mbetsa Chibule, visa hivyo viliongezeka zaidi msimu wa maambukizi ya virusi vya Corona, ambapo kaunti ya Kilifi iliorodheswa nafasi ya tatu nchini baada ya kaunti ya Bungoma na Samburu.
Chibule amesema kwa sasa ni asilimia 12.3 pekee ya visa hivyo vilivyoripotiwa tofauti na asilimia 30 wakati wa maambukizi ya Corona, akisisitiza kwamba juhudi hizo zimefanikiwa kupitia ushirikiano wa jamii na wadau mbalimbali.
Kiongozi huyo amedokeza kwamba serikali ya kaunti imetoa mafunzo kwa maafisa wa kutoa ushauri nasaha ili kusaidia kupambana na visa hivyo mashinani, akisema juhudi hizo zitaendelezwa sawa na kudhibiti madhila hayo.
Wakati uo huo ameweka wazi kwamba kaunti hiyo imekamilisha ujenzi wa sehemu salama ya kuwahifadhi watoto wanaopitia dhulma za kijinsia wakati kesi zao zikiendelea Mahakamani.