National News
Mahakama Kuu ya Malindi Yahairisha Kesi ya Ulaghai

Mahakama kuu mjini Malindi kaunti ya Kilifi imeahirisha kwa mara ya mwisho uamuzi wa kesi ya madai ya ulaghai wa fedha unaodaiwa kutekelezwa na Kenneth Njoroge Maina kwa mtalii Garallin Chiara.
Hakimu mkaazi wa Mahakama hiyo, Nkurrunah Namunyak amesema uamuzi wa kesi hiyo ulikuwa tayari ila mshtakiwa ameshindwa kufika Mahakamani kwa mara sita mfululizo kwa madai ya changamoto za kiafya.
Kulingana na stakabadhi za kesi hiyo, Maina anadaiwa kumlaghai Chiara shilingi 124,800 za kusimamia huduma za usafiri wa mtalii huyo kutoka Malindi hadi mbuga ya wanyama ya Tsavo na kukosa kutimiza ahadi yake.
Kupitia Wakili wa Maina, hapo awali alieleza Mahakama kwamba alikuwa amepata asilimia 70 ya fedha za mlalamishi na akataka kumrudishia Chiara fedha zake japo Mahakama hiyo ilidai kwamba wakili wa mshtakiwa alishindwa kuieleza Mahakama kuhusu ugonjwa wa mshtakiwa.
Uamuzi wa kesi hiyo unatarajiwa kutolewa mnamo siku ya Jumatatu tarehe 17 mwezi Machi mwaka huu.
National News
Chonga: Wakenya Wanaosafiri Ughaibuni Kusaka Ajira Hawazingatii Sheria za Leba

Mwenyekiti wa kamati ya Leba katika bunge la kitaifa Ken Chonga amesema baadhi ya wakenya ambao wanasafiri katika mataifa ya miliki za kiarabu kusaka ajira wamekosa kuzingatia sheria za Wizara ya Leba nchini na kuangukia mikononi mwa walaghai.
Chonga amesema ni lazima wakenya hao wachunguze mawakala wanaowasafirisha katika mataifa hayo kama wanatambulika na serikali, ndipo waingie katika mikataba ya uajiri ambayo imezingatia sheria za Leba nchini.
Akizungumza na Wanahabari mjini Kilifi, Chonga ambaye pia ni Mbunge wa Kilifi Kusini amesema ili wakenya waepuke madhila mbalimbali kutoka kwa waajiri wao katika mataifa hayo ni lazima wasafirishwe na mawakala waliosajiliwa na serikali.
Wakati huo huo amesema japo serikali iko mbioni kuhakikisha inawatafutia wakenya kazi katika mataifa ya ughaibuni ni lazima wanaosaka ajira za ughaibuni waingie katika mkataba wa uajiri kabla ya kusafiri nje ya nchi.
National News
Chibule: Visa vya Dhulma za Kijinsi Vimepungua Kilifi

Serikali ya kaunti ya Kilifi imesema visa vya dhulma za kijinsia katika kaunti hiyo vimepungua kwa kiwango kikubwa.
Kulingana na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Flora Mbetsa Chibule, visa hivyo viliongezeka zaidi msimu wa maambukizi ya virusi vya Corona, ambapo kaunti ya Kilifi iliorodheswa nafasi ya tatu nchini baada ya kaunti ya Bungoma na Samburu.
Chibule amesema kwa sasa ni asilimia 12.3 pekee ya visa hivyo vilivyoripotiwa tofauti na asilimia 30 wakati wa maambukizi ya Corona, akisisitiza kwamba juhudi hizo zimefanikiwa kupitia ushirikiano wa jamii na wadau mbalimbali.
Kiongozi huyo amedokeza kwamba serikali ya kaunti imetoa mafunzo kwa maafisa wa kutoa ushauri nasaha ili kusaidia kupambana na visa hivyo mashinani, akisema juhudi hizo zitaendelezwa sawa na kudhibiti madhila hayo.
Wakati uo huo ameweka wazi kwamba kaunti hiyo imekamilisha ujenzi wa sehemu salama ya kuwahifadhi watoto wanaopitia dhulma za kijinsia wakati kesi zao zikiendelea Mahakamani.