News
Wataalam wa uchumi samawati wakataa matumizi ya “Ring Net”

Wataalam wa maswala ya uchimi wa bahari nchini wamesistiza marufuku ya uvuvi wa kutumia nyavu aina ya Ring Net wakisema nyavu hizo zinaharibu zao la samaki baharini.
Wakiongozwa na Stanley Chai, wataalam hao walisema nyavu hizo zinafaa kutumika kuanzia umbali wa maili tano baharini kutoka ufuoni hali ambayo wavuvi wa kawaida hapa nchini kwa sasa hawana uwezo wa kufika umbali huo.
Chai alidokeza kuwa nyavu hizo zinapotumika hunasa mayai ya samaki baharini hali inayosambaratisha na kuharibu kizazi cha viumbe hai baharini.
“Watu wetu hawa wavuvi wadogo wadogo wanatumia ndoana, uvuvi wa ring net nitakwambia si uvuvi mzuri hasa kama utakuja kwa maji yasiyo ya kina kirefu, ring net inabeba mpaka mayai ya samaki, ukiona nakala ya sheria zetu ambazo hazijachapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali tumesema uvuvi wa ring net uruhusiwe umbali wa maili tano kuendelea na sio chini ya hapo kwa sababu chini ya hapo ndio samaki huzaana”, alisema Chai
Wakati huo huo Chai alisistiza umuhimu wa utekelezaji mpango wa kuingiza samaki nchini kutoka mataifa ya nje ili kuongeza kipato kupitia kodi na kuwezesha wavuvi kwa vifaa bora vya kuendeleza shughuli zao baharini.
“Wale samaki wakubwa tukiwaingiza hapa nchini tusiliseni ile ya dola elfu hamsini, hiyo ni kitu kidogo, yule samaki akiingizwa hapa nchini tunakusanya mabilioni, sasa hizi mabilioni tumesema nini kwa zile nakala ya sheria? tumesema zile pesa zitakazopatikana kwa biashara ya samaki asilimia 70 ziende kwa serikali kuu, asilimia 20 ziende kwa kaunti zinazopakana na bahari hindi, hii asilimia 10 iekezwe kuboresha wavuvi wadogowadogo halafu asilimia 10 ziende kwa vikundi vya maendeleo baharini-BMU, wale wavuvi moja kwa moja wanaweza kununua maboti makubwa nakupata uwezo wa kwenda kule chini”, aliongeza mtaalam Chai.
Kwa mda wavuvi eneo la pwani wamekuwa wakilalamikia serikali kuwafadhili na vifaa vya kisasa vya uvuvi ikiwepo boti zinazostahamili mawimbi baharini ili waweze kufika maji makuu na kuongeza pato la samaki.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Chrispus aomba msahama bunge la kaunti ya Taita Taveta

Mwakilishi wadi ya Bomani mjini Taveta kaunti ya Taita Taveta Chrispus Tondoo ameliomba bunge la kaunti hiyo msamaha kutokana na matamshi aliyoyatoa hapo awali akikashifu bunge hilo kwa madai ya kushamiri kwa visa vya ufisadi na utepetevu.
Tondoo akiomba msamaha katika bunge hilo alisema alitambua athari zilizosababishwa na matamshi hayo kwa wenyeji wa kaunti hiyo na bunge hilo, hali ambayo imemfanya kuchukua hatua hiyo ya kuomba msamaha.
Aidha Tondoo aliahidi kuliheshimu bunge hilo kwa mujibu wa kanuni na Sheria za bunge la kaunti ya Taita Taveta.
‘’Naomba msamaha kutokana na matamshi ambayo niliyatoa tarehe 2 na tarehe 3 mwezi wa Juni mwaka huu wa 2025 kwani hayakuwa yenye heshima kwa wenyeji wa Taita Taveta na bunge la kaunti’’, alisema Tondoo.
Tondoo alikuwa Mwakikishi wa wadi wa pili kuomba msamaha baada ya Mwakilishi wa wadi ya Kaloleni mjini Voi Ahmed Azari kuchukua hatua hiyo mwezi mmoja uliyopita.
Haya yalijiri baada ya kaimu spika wa bunge hilo Anselim Mwadime kuapa kuwachulia hatua za kisheria wanachama wanne wa bunge hilo, wawili wakiwa ni Tondoo na Azari ambayo tayari wameomba msamaha huku wawili wakiwa wamesalia bila kuomba msamaha.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mawakili Kilifi waungana kushtumu mauaji ya Wakili Mbobu

Siku chache baada ya Wakili Kyalo Mbobu kuuawa kinyama kwa kupigwa risasi mara kadhaa akiwa kwenye gari lake barabara ya Lang’ata jijini Nairobi, mawakili mjini Kilifi kaunti ya Kilifi wameungana na mawakili wengine nchini siku ya Ijumaa Semtemba 12 mwaka huu kufanya matembezi ya amani, wakishutumu vikali mauaji hayo.
Wakiongozwa na Mwakilishi wao Sesil Mila, mawakili hao walilaani vikali mauaji ya wakili Mbobu wakiishutumu serikali kwa kutowajibikia swala la usalama wa wananchi wake.
Aidha waliitaka idara ya usalama kuhakikisha kuwa inafanikisha wajibu wake wa kuwalinda mawakili wakisisitiza haja ya haki kupatikana kwa familia ya mwendazake wakili Kyalo.

Mawakili wa Kilifi wakiongozwa na Sesil Mila, washtumu mauaji ya Wakili Kyalo Mbobu
Mawakili hao sasa waliitaka idara ya upelezi na asasi zote husika kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina unafanywa kubaini watuhumiwa wa mauaji hayo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria haraka iwezekanavyo.
Taarifa ya Hamis Kombe