Business
Wafanyabiashara wa Soko la Matano Mane Waililia Serikali ya Kaunti ya Kilifi Kuwajengea Choo

Wafanyabiashara katika soko la Matano Mane, eneo la Vitengeni, Kaunti ya Kilifi, wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuwajengea choo, wakisema ukosefu wa huduma hiyo muhimu umekuwa kero kubwa inayozorotesha shughuli za biashara.
Wakiongozwa na Phelisia Mageshi, wafanyabiashara hao wamesema kuwa hali ya sasa imesababisha baadhi yao kuhamishia biashara zao nje ya soko hilo, kutokana na mazingira yasiyofaa kwa shughuli za kila siku.
Bi Mageshi ameeleza kuwa licha ya serikali ya kaunti kufahamishwa kuhusu changamoto hiyo mara kadhaa, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa, hali inayowafanya kuhisi kusahaulika.
Wameitaka serikali ya kaunti kuingilia kati kwa haraka ili kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na kuhakikisha afya ya wananchi inalindwa.
Business
Vijana Kaunti ya Tana River Waanzisha Biashara ya Sambusa za Samaki kuinua Uchumi

Vijana katika Kaunti ya Tana River wameanzisha biashara ya upishi wa sambusa za samaki kwa lengo la kujikwamua kiuchumi kwa kutumia rasilimali za baharini.
Wamebuni mbinu ya kipekee ya kuandaa sambusa kwa kutumia samaki wa aina mbalimbali, wakiwemo samaki papa. Mbali na sambusa, vijana hao pia wameweza kuunda bidhaa nyingine za thamani kutokana na samaki, hatua inayochochea ubunifu na kuongeza ajira miongoni mwao.
Kulingana na vijana hao, biashara hiyo inalenga kuongeza kipato chao na kufungua milango ya kuingia katika masoko mapya, ya ndani na hata ya nje ya kaunti.
Hatua hii imesukumwa na changamoto ya uhaba wa soko la samaki katika eneo hilo, hali ambayo husababisha uharibifu wa samaki kutokana na kukosa wanunuzi. Kwa hivyo, ubunifu huu umekuwa suluhisho la kiuchumi na kiteknolojia kwa vijana wa Tana River.
Business
Biashara ya Viazi Vitamu Yaendelea Kunga’ara Mjini Kilifi Licha ya Changamoto za Usafiri

Kilifi, Kenya – Wachuuzi wa viazi vitamu katika barabara ya mjini Kilifi wameripoti kuimarika kwa biashara hiyo ikilinganishwa na vipindi vya nyuma, wakisema hali hiyo imesababishwa na upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wingi kutoka mashambani.
Akizungumza na wanahabari, Joyce Kemboi, ambaye ni mmoja wa wachuuzi wa viazi vitamu katika eneo hilo, amesema kuwa kwa sasa wakulima wanavuna kwa wingi kutokana na hali nzuri ya mvua ambayo imeimarisha uzalishaji mashambani.
“Kwa sasa viazi vitamu vinapatikana kwa wingi sana, na hii imetuwezesha kufanya biashara nzuri. Wateja pia wameongezeka kwa sababu bidhaa ni safi na za bei nafuu,” amesema Kemboi.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, wachuuzi hao wanakabiliwa na changamoto ya gharama ya juu ya usafiri, hali inayochangiwa na kuharibika kwa barabara nyingi kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi.
Kemboi anasema kuwa usafirishaji wa viazi kutoka mashambani hadi sokoni umekuwa ghali mno, jambo ambalo linaathiri faida ya wachuuzi wa kiwango cha chini.
“Gharama ya kusafirisha gunia moja imepanda. Barabara nyingi zimeharibika, magari hayafiki kwa urahisi, na tunalazimika kutumia njia mbadala ambazo ni ghali,” ameongeza.
Kwa sasa, gunia la kilo 90 la viazi vitamu linauzwa kwa shilingi elfu 10, bei ambayo ni ya juu ikilinganishwa na msimu wa kiangazi ambapo gunia hilo hilo lingeuzwa kwa kati ya shilingi elfu 6 hadi 7.
Licha ya bei hiyo kupanda, wachuuzi wana matumaini kuwa soko litaendelea kuboreka hasa kwa kuwa bidhaa hiyo ina uhitaji mkubwa kwa wateja wa kila tabaka.