News
Viongozi wa Kilifi Wapinga Uekezaji wa Mradi wa Kawi ya Nuklia

Wizara ya Kawi nchini imefanya kikao cha mazungumzo na uongozi wa kaunti ya Kilifi, pamoja na wabunge na Wasimamizi wa Shirika la NUPEA kuhusu uekezaji wa mradi wa uzalishaji kawi ya Nuklia katika kijiji cha Uyombo wadi ya Matsangoni katika eneo bunge la Kilifi Kazkazini katika kaunti ya Kilifi.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kikao hicho mjini Kilifi, Waziri wa Kawi nchini Opiyo Wandayi amesema japo viongozi wa kaunti ya Kilifi pamoja na wananchi hawajaridhishwa na uekezaji wa mradi huo, mazungumzo kuhusu mradi huo bado yataendelea ili kuibuka na mwafaka kwani utasaidia pakubwa katika uzalishaji kawi.
Kwa upande wake Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro amesema msimamo wa serikali ya kaunti ya Kilifi pamoja na wananchi bado uko pale pale wa kuendelea kupinga uekezaji wa mradi huo wa mabilioni ya pesa, akisema utafiti uliofanywa umebaini kwamba mradi huo unaathari kubwa kwa wananchi.
Hata hivyo Mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya amesema kama viongozi kutoka kaunti ya Kilifi hawako tayari kupokea mradi huo wa uzalishaji kawi ya Nuklia, akisema changamoto nyingi bado hazitatuliwa katika mradi huo ambazo ni athari kwa wananchi.
Kikao hicho hata hivyo kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi, Mbunge wa Kaloleni Paul Katana, Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, Mbunge wa Ganze Kenneth Tungule, Katibu katika Wizara ya masuala ya vijana na michezo nchini Fikirini Jacobs miongoni mwa viongozi wengine.
News
Mvuvi aliyezama baharini Watamu apatikana Tanariver

Mwili wa mvuvi Hudhefa Laly aliyepotea baharini huko Watamu eneo bunge la Kilifi Kaskazini Kaunti ya Kilifi akiwa na ndugu yake Athman Laly umepatikana eneo la Shakiko -Mathole, kaunti ya Tana River.
Ndugu hao wawili walitoweka habarini siku ya Alhamisi 24, Julai 2025 katika bahari hindi wakati wakiendelea na shughuli zao za uvuvi.
Vitengo mbali mbali vya uokozi vimekuwa vikiendesha zoezi la kutafuta miili ya wawili hao kwa ushirikiano na wavuvi eneo la Watamu.
Kufikia sasa mwili wa Athman Laly kakake Hudhefa ungali haujapatikana huku juhudi za kuutafuta zikiendelea.
Jamii ya wavuvi katika eneo la Watamu ikiongozwa na kiongozi wa vijana Bakari Shaban iliiomba serikali ya kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa kununua boti za uokozi ili kusaidia kuokoa maisha wakati kunapotokea dharura baharini.
“Tunaomba tupate boti za kuokoa maisha baharini, popote alipo waziri Ali Joho angalau tupate boti za uokozi kama mbili hapa Watamu ni kitovu cha utalii kunamahoteli mengi, watalii wote wanaokuja Watamu mpaka leo hakuna boti za uokozi”, alisema Shaban.
Awali wao wazazi wa wavuvi waliopotea baharini Lali Athman Lali na Dhurai Mohamed Ali waliiomba serikali kuweka juhudi zaidi za kuwasaidia kuwapata wanawao kwani ndio tegemeo kubwa kwa familia yao.
“Uko usaidizi unatumika, kuna vijana wanaojitolea kwa maboti wanaenda ile sehemu ambayo wavuvi wanavua, wanajaribu kuzunguka lakini toka siku hiyo hawajapata chochote: Katika Maisha yangu mimi nawategemea hawa watoto kunisomeshea hawa watoto wangu ambao ni wadogo zao mashule, kwa chakula kwa hivyo naomba serikali inisaidie kwa sababu ndio tegemeo langu hao watoto”.walisema wazazi.
Kisa hiki kilijiri miezi kadhaa baada ya mvuvi mmoja kutoka eneo la Mnarani mjini Kilifi kufariki baharini baada ya kugongwa kichwani kwa pondo na wavuvi wenzake kulipotokea mzozo kuhusu pato la samaki.
Kufikia sasa mwili wa mvuvi huyo haujapatikana.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mombasa inaongoza kwa maambukizi ya MPOX nchini

Wizara ya afya nchini imesema kaunti ya Mombasa inaongoza kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa idara ya afya nchini Daktari Patrick Amoth, kaunti ya Mombasa imerekodi visa 139 kati ya visa 300 vilivyoripotiwa na wizara hiyo.
Amoth alidokeza kuwa serikali itatangaza siku maalum ya kutoa chanjo ya kudhibiti msambao wa ugonjwa huo wakishirikiana na shirika la afya ulimwenguni WHO.
Mkurugenzi huyo vile vile alimesema zoezi hilo litaambatana na hamasa kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi zaidi.
“Kwa wakati huu Mombasa ndio inaongoza kwa idadi ya visa 139 kwa hivyo tuchuke tahadhari kuhakikisha kwamba tunazuia maambukizi, na tunafanya mpango pamoja na shirika la afya duniani WHO, hapa tutakuja na mpango wa chanjo na ikifika huo wakati tunaomba watu wajitokeze wapate chanjo ili wapate kinga”,alisema Daktari Amoth.
Wakati huo huo Amoth aliokeza kuwa uchunguzi wa vifo vya watu wanne walioaga dunia wiki chache zilizopita huko Migadini, eneo bunge la Changamwe kaunti ya Mombasa umebaini walifariki kutokana na magonjwa mengine na wala sio maambukizi ya ugonjwa wa MPOX kama ilivyodhaniwa na wakaazi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.