News
Viongozi wa dini wamkosoa Kithure Kindiki.

Viongozi wa dini ukanda wa wamemkosoa naibu rais profesa Kithure Kindiki kuhusiana na kauli yake kwamba baadhi ya viongozi wa dini na wanadiplomasia walihusika katika kuunga mkono maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z ya mwezi juni 25 2025.
Mwenyekiti wa kitaifa wa baraza la kuu la waislamu SUPKEM Sheik Muhdhar Khitamy alisema matamshi ya Kindiki ni siasa zinazolenga kuwanyooshea lawama viongozi wengine.
Sheikh Kitamy alisema kuwa kwa sasa wanasiasa wamekuwa na usemi mkubwa kutokana na hulka ya kuwahonga wananchi na kuwafanya viongozi wa dini kutosikizwa.
Akizungumza na wanahabari kiongozi huyo wa dini ya kiislamu alionya kuwa iwapo wakenya hawatakuwa makini, kunauwezekano wa taifa kuelekea pabaya kutokana na vijana kutumiwa vibaya na wanasiasa.
“Ukweli wa mambo ni kwamba wanasiasa wanachukuwa jukumu kubwa sana kwa sababu ya pesa za kuwatumia watu, jambo lolote liwe la kikatiba au nini utaona linawahusisha hao wanasiasa, twawaambia wanasiasa hao ndio chumvi, watengeneze nchi, watakuja kujuta kwasababu hali inavyokwenda ni mbaya”, alisema Khitamy.
Naye mwakilishi wa vijana katika baraza hilo Abdhulmalik Ali aliwataka vijana nchini kuwa makini na kufuata ushauri wa kisheria iwapo hawajaridhishwa na utendakazi wa viongozi.
Ali vile vile aliwashinikiza vijana kuepuka maandamano ya vurugu.
“Wanasiasa tuchungane nao, niwatu wanamaslahi yao zaidi ya wewe kijana, hii kenya inakuhitaji wewe kijana, kama kiongozi anatufaa tumpigie kura muhula ujao, kama hatufai njia iko ya kumtoa lakini sio suala la kumwaga damu”, alisema Abdhulmalik.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi