News
Ujenzi wa barabara ya Kibaoni-Ganze-Bamba umeng’oa nanga

Baada ya wakaazi wa eneo bunge la Kilifi Kaskazini na Ganze kulalamikia ubovu wa barabara ya Kibaoni-Ganze hadi Bamba na kuangziwa na wanahabari, hali sasa ni tofauti.
Ujenzi wa barabara hiyo iliyoshudia utata na maandamano, sasa unaendelea huku mkandarasi akiwa katika hatua kupiga msasa barabara na kujenga mabomba na sehemu za kupitisha maji hasa kunaponyesha.
Justine Kandie ni muangalizi wa ujenzi wa barabara hiyo, alisema shughuli hiyo imegawanywa mara mbili, na kwa sasa wameanza ujenzi wa barabara hiyo kutoka eneo la Kibaoni mjini Kilifi kuelekea Ganze.
Kandie alisema mpango huo ulianza mwaka 2021 kutoka eneo bunge la Ganze kuelekea kibaoni japo ulisitishwa wakati huo na sasa wameanza tena kujenga umbali wa kilomita tano.
“Katika awamu ya kwanza kwa mwaka wa 2021 tulianza barabara kutoka Ganze tulikuwa tunafanya kilomita tano, kwa mda wa miaka miwili barabara ikasimama kidogo, baadaye kurudi kwa huu mwaka wa 2025 ndio tumepewa kile kiwango tuanze kutoka kibaoni kuelekea Ganze, katika hii awamu ya pili tunafanya kilomita tano ila kwa sababu barabara ni mbovu tumeamua kuanzia huku kwa Kimanje tukielekea Kibaoni ili barabara yetu iwe sawa wakati tunaposafirisha vifaa vya ujenzi”,alisema Kandie.
Baadhi ya mafundi wakiendelea na ujenzi wa barabara ya kuelekea Ganze
Picha:(Joseph Jira)
Kandie pia alisema mda wa miaka miwili aliopewa mkandarasi kukamilisha ujenzi huo wa barabara utategemea na mgao wa pesa zitatakaotolewa kufanikisha mradi huo.
“Ule mda wa kukamilisha barabara huwa inategemea uwezo wa mwanakandarasi kama ako na fedha za kutosha, itamsaidia kukamilisha kwa mda unaofaa, kwa sababu hii barabara yetu walikuwa wametupa kama miaka miwili ila saa hii mda umesonga”, aliongeza Kandie.
Wakaazi pamoja na wahudumu wa uchukuzi wa umma wanaotumia barabara hiyo wameeleza matumaini ya kuimarika kwa sekta ya uchukuzi sawa na uchumi mara tu ujenzi utakapokamilika.
Itakumbukwa kwamba barabara hiyo ilileta utata na kusababisha wakaazi kuandamana na kuifunga sawa na kutatiza shughuli za usafiri kwa mda.
“Hapo kwa usafiri na biashara huenda kukabadilika kwa sababu wengi pia wanakataa huku kwa sababu yah ii barabara vile ni mbovu hasa kazi zinakuwa ziko chini kwa sababu ya vumbi”,alisema Jeremiah Mwaringa
Tinga tinga za ujenzi wa barabara ya kuelekea Ganze.
Picha:(Joseph Jira)
Mvutano huo pia ulishuhudiwa baina ya mbunge wa Ganze Kenneth Kazungu Tungule na mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kuhusu ujenzi wa barabara unakofaa kuanza kutekelezwa.
Hata hivyo muangalizi wa mradi huu aelieleza matumaini yake kuwa mvutano huo wa wanasiasa hautaathiri utendakazi wao huku akishinikiza wahudumu wa barabara hiyo kuwa na uvumilivu wakati wanapoendelea na ujenzi huo.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Godhana, awataka wakaazi kutoingiza siasa miradi ya maendeleo

Gavana wa kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kujiepusha na wanasiasa ambao wanaingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo.
Godhana alisema hilo limechangia kaunti ya Tana River kusalia nyuma kimaendeleo hali ambayo itasababisha miradi mingi kuzidi kukwama.
Godhana alisema ni lazima viongozi na wenyeji wa kaunti ya Tana River washirikiane na uongozi wa kaunti ili kuafikia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo Godhana aliesema mradi wa Village Cluster ambao umekuwa ukipingwa ndio utakaosaidia kudhibiti changamoto ambazo zinaikumba kaunti ya Tana River.
Naye Mahat Ali Loka ambaye ni Naibu Gavana wa kaunti ya Tana River, aliwaonya wanasiasa kutoka kaunti zingine dhidi ya kuingilia siasa za kaunti hiyo huku Spika wa bunge la kaunti hiyo Osman Noor Galole, akitoa onyo kwa wafanyikazi wa umma dhidi ya kujumu la serikali ya kaunti ya Tana River.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mwili wapatikana baharini Shelly Beach Likoni

Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamme ambaye hajafahamika umepatikana ukielea katika maji ya bahari hindi kwenye ufuo wa Shelly Beach eneo bunge la Likoni.
Ripoti ya polisi ilibaini kuwa mwili huo uligunduliwa na wavuvi eneo hilo, ambao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Shelly Beach kuhusiana na tukio hilo.
Polisi walisema hawakubaini mara moja anakotoka mtu huyo.
Vile vile haikubainika iwapo marehemu alizama au aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa baharini.
Polisi walisema hawajakutana na stakabadhi zozote za kumtambulisha mtu huyo huku wakiwasihi wananchi kutoa taarifa iwapo wanafahamu familia ya marehemu.
Mwili unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Rufaa ya Coast General Mombasa wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Joseph Jira