News
Uhaba wa maji wakera wakaazi Mombasa

Wakaazi wa mtaa wa mabanda wa Bangladeshi eneo bunge la Jomvu, kaunti ya Mombasa, wanalalamikia uhaba mkubwa wa maji unaoendelea kushuhudiwa kwa zaidi ya mda wa wiki tatu sasa.
Wakiongozwa na Betty Achieng’, wakaazi hao walisema hali hiyo imeathiri pakubwa shughuli zao za kila siku.
Walisema bei ya maji imeongezeka mara dufu kutokana na uhaba huo.
Aidha walisema wanalazimika kununua maji kutoka kwa wauzaji wa rejareja, wanaotumia mikokoteni huku wakihofia usalama wa maji hayo, hasa katika matumizi ya nyumbani.
“Tunaomba msaada kwa serikali itusaidie kwa mambo ya maji, angalia vile tunahangaika hata kazini hatuendi kwa sababu vitu vyetu ni vichafu, tuko na watoto wadogo, nguo ni chafu, saa zingine tunakaa hapa tunakaa hapa tunangoja msaada wa maji”, walisema wakaazi hao
Kwa upande wao, maafisa kutoka wizara ya maji ya kaunti ya Mombasa walieleza kuwa tatizo hilo linatokana na upungufu wa maji katika kituo cha kusambaza maji cha Baricho kaunti ya Kilifi, hali iliyosababisha maeneo mengi ya kaunti hiyo kukosa bidhaa hiyo muhimu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.
News
Washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu wakamatwa, Malindi

Maafisa wa polisi Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wamewanasa washukiwa 42 wa magenge ya uhalifu katika msako kwenye mitaa ya Karima, Soweto, Milano na Mgandini.
Polisi ilisema msako huo umewawezesha kuwakamata washukiwa 11 wa genge la “Wakali Mwisho” na wanawake watano kwa visa vya utovu wa nidhamu.
Msako huo unafuatia zaira ya kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno katika eneo hilo na kuwataka polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na wanachama wa magenge hayo wanaoendelea kuwahangaisha wananchi.
Simu 14 zilizoshukiwa kuwa za wizi zilinaswa kutoka kwa mshukiwa Ahmed Ali.
Magenge ya uhalifu wakiwemo wale wanaojiita mawoza ni miongoni mwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama miongoni mwa wakaazi eneo hilo.
Idara ya usalama ilikuwa mbioni kuwasaka wahalifu katika mji huo wa kitalii katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi na kutekeleza vitendo vya wizi.
Taarifa ya Joseph Jira.
News
Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuchangia mapato duni ya samaki, Lamu

Wadau katika sekta ya mazingira kaunti ya Lamu wanasema mabadiliko ya hali ya anga yanayoshuhudiwa sawa na ujenzi wa bandari ya Lamu kumechangia mapato ya samaki kupungua katika bahari hindi.
Mahmoud Yusuf ambaye ni mwanazingira alisema zana za kizamani wanazotumia wavuvi kuvua samaki pia zinachangia mapato duni ya samaki.
Yusuf alisema tangu ujenzi huo wa bandari uanze, maji ya bahari chini yamekuwa na matope kutokana na kuchimbwa na kufukuliwa kwa bahari, hali iliyochangia samaki kutorokea bahari kuu.
Mwanamazingira huyo aliitaka serikali kuwapa wavuvi vifaa vya kisasa vya uvuvi sawa na meli za uvuvi zitakazowawezesha kufika maji makuu, baada ya bandari ya ndani kuharibika.
Taarifa ya Joseph Jira.