Sports
Sinner na Alcaraz Wakutana Tena Fainali ya Cincinnati Baada ya Ushindi

Mchezaji Tenesi Nambari moja duniani Jannik Sinner na mpinzani wake mkali Carlos Alcaraz watakutana tena katika fainali kubwa kwa mara ya nne msimu huu baada ya wote wawili kufanikisha ushindi wa seti za moja kwa moja na kufuzu fainali ya ATP-WTA Cincinnati Open wikendi.
Bingwa mtetezi Sinner alimzima kwa ukali mchezaji wa kufuzu aliyeorodheshwa nambari 136 duniani Terence Atmane kwa 7-6 (7/4), 6-2, huku Alcaraz, aliyeshika nafasi ya pili kwa ubora, akimshinda Alexander Zverev aliyekuwa akiteseka na joto na unyevunyevu wa nyuzi joto 32 kwa 6-4, 6-3.
Alcaraz na Sinner tayari wamekabiliana kwenye fainali msimu huu huko Rome, Roland Garros na Wimbledon, ambapo Muitaliano alishinda mchezo wao wa mwisho katika All England Club mwezi uliopita.
Sinner, akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 24, aliua ndoto ya Mfaransa Atmane na sasa anawinda kuwa mwanaume wa kwanza tangu Roger Federer (2014-15) kushinda taji la Cincinnati mfululizo. Huu ukiwa ni mashindano yake ya kwanza tangu alipotwaa ubingwa wa Wimbledon, hajapoteza seti yoyote akielekea fainali.
“Kila mara unapokutana na mpinzani mpya ni changamoto ngumu sana,” alisema Sinner. “Katika hatua za mwisho za mashindano, shinikizo huwa kubwa na kila mmoja anastahili kuwa hapo.”
Kwa upande mwingine, Alcaraz atakuwa akicheza fainali yake ya pili ya Cincinnati baada ya kupoteza dhidi ya Novak Djokovic mwaka 2023.
Mhispania huyo sasa ameongeza idadi ya ushindi wake msimu huu kwenye mashindano ya ATP hadi michuano 53, akiwa tayari ameshinda mataji matano mwaka huu.
Sports
Shirika la Kupiga Vita Dawa za Kusisimua Misuli Duniani (WADA) Lawashtaki Kenya kwa Kukosa Kutii Kanuni

Shirika la Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli Duniani (WADA) siku ya Alhamisi limeshtaki Kenya kwa kutotii masharti yake, hatua inayoweza kusababisha nchi hiyo ya Afrika Mashariki kuwekewa vikwazo mwezi ujao.
WADA, lenye makao yake Montreal, Canada, limesema kuwa shirika la kitaifa la kudhibiti matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini Kenya bado halijashughulikia mahitaji muhimu yaliyoainishwa baada ya ukaguzi uliofanywa mwezi Mei 2024.
Kwa sasa, Kenya ina siku 21 za kupinga madai hayo au kufanya marekebisho yanayohitajika na WADA, la sivyo itatangazwa rasmi kuwa imekosa kutii kanuni.
Kwa sasa, kuna wadau wanne waliotia saini kanuni za WADA walioko kwenye orodha ya kutotii masharti. Hawa ni pamoja na:
-
Urusi
-
Sri Lanka
-
Shirikisho la Kimataifa la Basque Pelota
-
Shirikisho la Kimataifa la Mazoezi ya Mwili na Ujenzi wa Misuli (IFBB)
Sports
Mkurugenzi Mkuu wa Cricket Kenya Ronald Bukusi Afafanua Hali ya Ukocha katika Timu ya Taifa

Mkurugenzi Mkuu wa Cricket Kenya, Ronald Bukusi, ameondoa uvumi kuhusu mpangilio wa uongozi ndani ya timu ya taifa ya kriketi ya wanaume, akisisitiza kuwa hakuna mkanganyiko wowote kuhusu majukumu ya makocha Joseph Angara na Lameck Onyango.
Akizungumza katika makao makuu ya shirikisho hilo Ruaraka, Nairobi, Bukusi alieleza kuwa benchi la kiufundi linafanya kazi kwa mshikamano, huku wachezaji hao wa zamani wa kimataifa wakikamilishana katika uwezo wao.
“Tuna makocha wawili. Inategemea tu wanachofanya siku hiyo maalum,” alisema Bukusi.
Kwa sasa, Angara ndiye kocha mkuu, huku Onyango akiwa msaidizi wake. Wawili hao walichukua majukumu hayo kwa muda tangu Septemba 2024 baada ya bodi kufuta uteuzi wa mchezaji wa zamani wa India, Dodda Ganesh, kwa sababu za ukiukaji wa taratibu.
Kwa kuzingatia kuwa mashindano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la ICC la 2027 yanakaribia, Bukusi alisisitiza kuwa timu ya taifa imedhamiria kazi iliyo mbele yao. Mashindano hayo makubwa duniani yataandaliwa kwa pamoja na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.
“Kwa sasa, malengo yetu ni kujaribu kufika Zimbabwe na kufuzu Kombe la Dunia,” alisema Bukusi. “Tuna benchi bora la kiufundi linaloongozwa na Bw. Tariq [mwanabodi], na kwa pamoja tunashughulikia changamoto zinazoikumba timu.”
Hata hivyo, alionya kuwa mafanikio yanahitaji zaidi ya kipaji cha uwanjani, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na utiifu wa kanuni katika mifumo yote.
“Lazima tuwe watiifu kuhusu fedha na kupiga vita matumizi ya dawa za kusisimua misuli. Sio kitu cha kufanikisha mara moja—itakuwa mchakato,” aliongeza.
Kenya itaendeleza kampeni ya kufuzu kwa kuikabili Namibia Septemba 26 katika Harare Sports Club, kisha kucheza dhidi ya Malawi Septemba 28 katika Takashinga Cricket Club. Mechi yao ya mwisho ya makundi itakuwa dhidi ya Nigeria Septemba 30.
Kenya inatarajia kurudia historia ya mwaka 2003, walipofika nusu fainali, mafanikio makubwa zaidi kuwahi kupatikana na taifa lisilocheza mechi za Test.