News
Rais Ruto atuma KDF kusimamia ujenzi wa hospitali nchini

Rais William Ruto ametuma jeshi la KDF kusimamia ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 75 kote nchini katika juhudi za kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa haraka.
Akizungumza katika kaunti ya Narok wakati wa uzinduzi wa hospitali ya Sogoo Level 4, waziri wa ulinzi Patrick Mariru alifichua kuwa ujenzi wa hospitali hiyo yenye mamlaka kamili itakamilika baada ya mda wa miezi 11.
Ujenzi wa hospitali ya Sogoo Level 4 ulivutia rais Ruto alipozuru eneo hilo mwezi mei mwaka 2025, jambo lililomfanya kuagiza KDF kuipandisha hadhi.
Mariru hata hivyo alishikilia kuwa wafanyikazi wote wasio na ujuzi watatolewa kutoka kwa jamii.
“Jeshi litamsimamia mkandarasi. Hilo liwe wazi, kazi yote itafanywa na vijana wa Sogoo. Tutaweka maafisa wawili na kila jioni watanipa ripoti ya maendeleo,” alisema Mariru.
“Tuna zaidi ya miradi 75 tunayosimamia na sio kwamba tunabadilisha wakala wa serikali tunataka tu kushirikiana na ofisi tofauti miongoni mwao wizara za afya na michezo.”
Taarifa ya Joseph Jira
News
Wahudumu wa afya Lamu watishia kuishtaki serikali ya kaunti hiyo

Wahudumu wa Afya kaunti ya Lamu wametishia kuelekea Mahakamani kuishtaki serikali ya kaunti hiyo kwa kukaidi kutekeleza matakwa yao.
Wahudumu hao waliishtumu serikali ya kaunti ya Lamu kwa kupuuza matakwa yao na badala yake kutumia vitisho ili kuwashurutisha kurejea kazini.
Kulingana na viongozi wa wahudumu hao, licha ya mgomo wao kuendelea kwa zaidi ya wiki mbili serikali ya kaunti hiyo imekataa kata kuandaa vikao vya kusuluhisha malalamishi yao.
Baadhi ya changamoto wanazolalamikia ni pamoja na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kupandishwa vyeo, kupuuzwa kwa mkataba wa makubaliano ya nyongeza ya mishahara, kunyimwa kwa mishahara kwa baadhi ya wahudumu hao miongoni mwa matakwa mengine.
“Mkiendelea kutufinyilia itabidi tufuate njia ya sheria kwa sababu tunajua tunalilia haki yetu, haiwezekani serikali ya kaunti inashindwa kutupandisha vyeo ilhali tumefanya kazi kwa miaka 15 sasa, hatuwezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira duni na pia mkataba wa makubaliano kuhusu nyongeza ya mishahara sharti itekelezwe” walisisitiza viongozi hao.
Wakati uo huo serikali ya kaunti ya Lamu imejibu malimishi yao kupitia barua na kutangaza kuwa mgomu huo ni kinyume cha seria na kuwataka wahudumu hao kurejea kazini mara moja.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Wahadhiri watishia kushiriki mgomo wa kitaifa

Muungano wa Wahadhiri wa vyuo vikuu nchini UASU umetoa matakaa ya siku 7 kwa serikali kutimiza matakwa yao la sivyo watishiriki mgomo wa kitaifa.
Wahadhiri hao walisema iwapo serikali itaendelea kukaidi suala hilo basi watasambaratisha shughuli za masomo ya vyuo vikuu 41 kote nchini.
Muungano huo wa UASU, uliilaumu serikali kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya pamoja nyongeza ya mishahara ikiwemo malimbikizi ya shilingi bilioni 10 tangu mwaka wa 2017.
Wakiongozwa na Katibu mkuu wa Muungano wa UASU Constantine Wasonga, Wahadhiri hao walilalamika kwamba serikali imeshindwa kutekeleza awamu ya pili ya nyongeza ya mishahara ya mwaka wa 2021 hadi 2025.
“Tumetoa onyo kwa serikali hadi tarehe 17 mwezi huu wa Septemba iwe imetimiza matakwa yetu yote ya mkataba wa makubaliano wa CBA mwaka wa 2017 wa shilingi bilioni 10 na pia tufanye mazungumzo na serikali kuhusu mkataba wa makubaliano wa malipo CBA wa mwaka wa 2021 hadi 2025”, alisema Wasonga.
Wahadhari hao walishikilia kwamba kuna masuala mengi ibuka ambayo serikali haijatimiza na imekuwa ikitoa ahadi kila mara, wakisema kwamba ni lazima serikali kupitia Wizara ya Elimu nchini kutimiza ahadi hizo kwa wakati.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi