News
Nassir, Awaonya Vijana Wanaojihusisha na Uhalifu Mombasa

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amekashifu vikali ongezeko la vijana wadogo wanaoendeleza uhalifu katika kaunti hiyo.
Abdulswamad amewakosoa wale wanaosema kuwa vijana hao wanatekeleza uhalifu kutokana na ukosefu wa ajira, akisema wengi wa vijana hao ni wa umri mdogo.
Aidha amekariri kuwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18 hawawezi kupewa ajira, akisema ni sharti wazazi wawajibike katika malezi ya watoto wao ili kuwaepusha dhidi ya utovu wa maadili.
Kauli yake imeungwa mkono na Mwenyekiti wa baraza la kitaifa la ushauri kwa waislamu KEMNAC, Sheikh Juma Ngao ambaye amesema wazazi wengi wamezembea katika kuwalea watoto wao hali inayowasababishia vijana hao kujiingiza katika uhalifu.
Sheikh Ngao amependekeza vijana hao wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria pasi na kujali umri wao.
News
Macharia: Jamii ya Kilifi kusini watapeliwa ardhi kufuatia ukosefu wa Elimu

Msaidizi wa Kamishna wa kaunti ya Kilifi eneo la Kilifi Kusini, Francis Macharia amesema ukosefu wa elimu umechangia kwa wanajamii wengi kaunti ya Kilifi kutapeliwa katika umiliki wa ardhi.
Akizungumza eneo la Vipingo, Macharia alisema kuwa wanajamii wengi hasa wazee wamekuwa wakitapeliwa mashamba yao kutokana na kukosa kisomo.
Macharia alisisitiza haja ya jamii kuzingatia elimu kwani visa vya ulaghai wa mashamba kutokana na ukosefu wa elimu vimekithiri mno hasa mashanani.
“Kuna baadhi ya vijana pia wamekuwa wakiwatapeli wazazi wao fedha za inua jamii pindi zinapotumwa, na hii imechangiwa na kutosoma wazee hao” aliongeza Macharia.
Macharia alisema wazazi pia wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanao wanapata elimu ipasavyo akisema kuwa eneo la Kilifi kusini limekuwa na visa vingi vya watoto wanaoacha shule na kuingilia vibarua.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Makalo atoa wito kwa serikali kuendeleza mpango wa ugavi wa chakula

Mwakilishi wa wadi ya Kasighau kaunti ya Taita Taveta Amos Makalo ametoa wito kwa serikali kuu kuendeleza mpango wa ugavi wa chakula cha msaada katika eneo hilo sawa na maeneo mengine kote nchini ili kunusuru maelfu ya wananchi wanaokabiliwa na baa la nja.
Makalo alisema chakula hicho ni kidogo mno kwani wananchi wengi wa Kasighau pamoja na maeneo mengine ya kaunti hiyo wanakabiliwa na baa la njaa.
Wakati huohuo Makalo alimshinikiza mwakilishi wa kike kwenye kaunti hiyo Lydia Haika kuishawishi serikali kuu kuikumbuka kaunti hiyo katika kupeana misaada mbalimbali ambayo itawafaidi wenyeji.
“Wananchi wanahangaika kutokana na njaa. Na kwasababu umetutembelea na mazuri leo wacha niombe kwamba hayo Mazuri yaendelee kwa muda huu ulio mbele yetu maana hali ni ngumu sana’’
Haya yanajiri huku Serikali ya kitaifa kupitia wizara ya huduma za kitaifa na mipango maalum ikiendeleza shughuli za usambazaji wa chakula cha msaada kwa wahanga wa baa la njaa kaunti ya Taita Taveta na maeneo mengine nchini.
Taarifa ya Janet Mumbi