News
Murkomen: serikali itaongozwa na usalama wa kitaifa, sio amri za mahakama.

Mamlaka ya mawasiliano nchini CA imeondoa amri ya kuzuia vituo vya redio na televisheni kuweka mubashara matangazo kuhusu maandamano.
Uamuzi huo ni kufuatia amri ya mahakama iliyokosoa hatua ya mamlaka hiyo mbali na kuzima mawimbi ya vituo vya runinga tatu za televisheni nchini.
Hata hivyo waziri wa usalama wa kitaifa Kipchumba Murkomen alisema serikali itaongozwa na usalama wa kitaifa na wala sio amri za mahakama akiongeza kuwa hajutii uamuzi wa kuzima mawimbi ya vituo hivyo.
CA ilitangaza uamuzi huo kufuatia amri ya mahakama iliyotolewa na majaji wawili John Chigiti na Chacha Mwita kufuatia ombi lililowasilishwa mahakamani na shirika la katiba institute, na tume ya kitaifa ya haki za binadam vile vile chama cha mawakili LSK.
Kulingana na Murkomen Vyombo vya habari vilisaidia kuwachochea waandamanaji.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mahakama kuu yatupilia mbali ombi la Gachagua

Mahakama kuu imetupilia mbali ombi la pili la aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua la kutaka jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi ya kupinga kubanduliwa wake mamlakani kuzuiliwa kuskiza kesi hiyo.
Gachagua alisema kwamba majaji hao watatu akiwemo Jaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Fridah Mugambi wanafaa kuondolewa kwenye kesi hiyo kwa misingi kwamba uteuzi wao haujazingatia sheria.
Mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi hilo, na kusema kwamba jopo hilo la majaji watatu liliteuliwa na Jaji mkuu Martha Koome kwa kuambatana na sheria na kanuni za idara ya Mahakama.
Mahakama imeshikilia kwamba jopo hilo la majaji wa Mahakama kuu litaendelea kusikiliza kesi hiyo hadi wakati wa kutoa uamuzi kwa kuzingatia sheria, na kanuni za idara ya Mahakama pamoja na Katiba ya Kenya.
Mahakama hiyo pia ilitupilia mbali ombi la Mwanaharakati Fredrick Mula ambaye alitaka kubadilishwa kuwa mlalamishi katika kesi nne za kuondolewa mashtaka dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambazo alikuwa amewasilisha awali na kisha kutaka kujiondoa.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Wazee wa Kaya wanataka bunge kupitisha sheria kudhibiti mauaji ya wazee

Muungano wa Wazee wa Kaya kaunti ya Kilifi umeitaka serikali kuu kupitia bunge la kitaifa kubadilisha sheria ya mwaka wa 1926 kuhusu uchawi ili kuwezesha utamaduni kudhibiti mauaji ya wazee yanayoendelea kushuhudiwa kaunti ya Kilifi.
Wakiongozwa na Stanley Kahindi Kiraga wamesema kuwa sheria hiyo imechangia pakubwa mauaji ya wakongwe Kilifi kutokana na swala kuwa haitambui uwepo wa uchawi na jinsi ya kuudhibiti.
Kiraga sasa anasema ni sharti sheria hiyo iondolewe au ifanyiwe ukarabati bungeni hali itayopelekea uchawi kudhibitiwa kupitia mila na utamaduni.
“Vijana wanaowaua wazee wakiwasingizia kuwa wachawi wanazidi kuongezeka na kwa sababu hakuna sheria ya moja kwa moja ya kuwashtaki na kuwafunga” amesema Kiraga akieleza kusikitishwa kwake na ongezeko la magenge ya vijana wanaolipwa kutekelezwa mauaji ya wazee kwa shutuma za uchawi.
Taarifa ya Hamis Kombe