News
Mashirika ya kiserikali yaagizwa kutoa huduma kielektroniki.

Mkuu wa utumishi wa umma nchini Felix Koskei, ameagiza mashirika yote ya serikali kuanza kutoa huduma za ununuzi kupitia mfumo wa kielektroniki wa serikali almaarufu e-GP mara moja.
Koskei alisema agizo hilo linafaa kutekelezwa kikamilifu bila kuchelewa, akisistiza kuwa ndiyo njia pekee ya kuhakikisha uwazi na kujenga imani ya umma.
Koskei alidokeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuepusha visa vya ufisadi ambao umewanyima wananchi fursa ya kunufaika na huduma za serikali.
Mkuu huyo wa utumishi wa umma pia aliwataka wasimamizi wa mashirika ya serikali kuzingatia uadilifu na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao, na kuhakikisha mashirika hayo ya umma yanahudumu ipasavyo ili kufanikisha malengo ya serikali.
Aliyasema hayo kwenye mkutano uliowaleta pamoja makatibu wa wizara, wakuu wa mashirika ya serikali na asasi nyingine za usimamizi, ili kushughulikia masuala muhimu katika idara ya utumishi wa umma.
Taarifa ya Janet Mumbi.
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi