News
Mashirika ya kijamii yaelimisha umma kuhusu athari za mazingira

Mashirika mbalimbali ya kijamii kaunti ya Kilifi yanayojihusisha na masuala ya uchumi wa bahari yamejitokeza na kuhamasisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya anga.
Mpango huo unaoendelezwa na mataifa 5 barani Afrika ikiwemo Kenya, Comoros, Madagascar, Tanzania na Msumbiji, unalenga kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya anga, ambapo nchini Kenya maeneo ya Magarini, Malindi na Kilifi kaskazini unaendelezwa.
Mashirika hayo yakiongozwa na Shirika la Mission Inclusion na Groots Kenya yalifichua kwamba ongezeko la viwango vya chumvi baharini vimechangia pakubwa kushughudiwa kwa idadi ndogo ya samaki baharini.

Wadau wa masuala ya uchumi wa bahari wakongamana Watamu
Hata hivyo wakaazi waliohudhuria Kongamano hilo walishauriwa kuendeleza upanzi wa mikoko katika maeneo ya bahari kama njia mojawapo ya kudhibiti mazingira ya bahari.
Mpango huo ulioanzishwa mwezi Mei mwaka wa 2023 unalenga kuwafikia watu elfu 85 kwa kipindi cha miaka 3.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Gavana Sakaja aponea shoka la kutimuliwa mamlakani

Mchakato wa kumbandua mamlakani Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja pamoja na Naibu wake James Muchiri umekosa kuendelea baada ya Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga kuingilia kati mchakato huo.
Hii ni baada ya Odinga pamoja na viongozi wakuu wa chama cha ODM na Wawakilishi wadi wa kaunti ya Nairobi kufanya kikao cha mazungumzo kwa masaa kadhaa na kuibuka na suluhisho la kusitishwa kwa mchakato huo.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kikao hicho kilichoandaliwa jijini Nairobi, Mbunge wa Makadara George Aladwa alisema kikao hicho kimasikiliza lalama zote zilizoibuliwa na wawakilishi wadi hao dhidi ya Gavana Sakaja na kuafikia masuala kadhaa.
Aladwa alisema Gavana Sakaja amehimizwa kurekebisha masuala yalioibuliwa na Wawakilishi wadi hao sawa na kushirikiana naoi li kuhakikisha kaunti ya Nairobi inapiga hatua kimaendeleo na wananchi wa kaunti hiyo wananufaika.
Siku ya Jumatatu Septemba 1, 2025, Wawakilishi wadi hao wa Nairobi wakiongozwa na Mwakilishi wadi ya Kileleshwa Robert Alai, walisema Gavana Sakaja alishindwa kuwajibikia majukumu yake kama Gavana na kwamba hafai kushikilia wadhfa huo.
Wawakilishi wadi hao waliorodhesha malalamishi zaidi ya 20 dhidi ya Gavana Sakaja ikiwemo uongozi duni, ukiukaji wa Katiba, usimamizi duni wa jiji la Nairobi, kuporomoka kwa majengo kiholela, mirundiko ya taka katikati wa jiji, huduma duni za afya, miongoni mwa masuala mengine.
Wawakilishi wadi hao walisema wako na ushahidi wa kutosha dhidi ya Gavana Sakaja, wakishikilia kwamba Gavana huyo ameshindwa kusimamia jiji la Nairobi, wakipendekeza kutimuliwa Mamlakani pamoja na Naibu wake James Muchiri.
Itakumbukwa kwamba Wawakilishi wadi zaidi ya 100 walikuwa tayari wametia saini hoja ya kumbandua mamlakani Gavana Sakaja pamoja na Naibu wake James Muchiri kwa madai ya kushindwa kuwajibikia majukumu yao miongoni mwa hoja zengine zaidi ya 20 lakini hatua ya Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga kuingilia kati suala hilo kulimnuru Gavana Sakaja.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Wazazi walalamikia mazingira duni ya Elimu, Magarini

Wazazi katika shule ya msingi ya Tangai eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi wanaiomba serikali pamoja na wahisani kubuni mikakati ya kuboresha miundomsingi ya taasisi hiyo ya elimu hasa majengo ya shule.
Wazazi hao wakiongozwa na Thomas Kombe, walisema baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo hulazimika kuhamia shule nyingine punde wanapofika gredi ya kwanza kutokana na uhaba wa madarasa.
Kombe ambaye pia ni kiongozi wa vijana eneo hilo alilitaja suala la uhaba wa walimu shuleni kama changamoto, akisema shule hiyo ina mwalimu mmoja pekee na madarasa mawili.
“Shule iko lakini ni ndogo hakuna gredi ya kwanza na ya pili hawaweze kutoka Tangai hadi Shaurimoyo na kuna baridi ambayo inafanya watoto wanadhohofika kiafya. Tunaiomba serikali na wahisani watusaidie kuboresha shule yetu”, alisema Kombe.
Wakati uo huo aliiomba serikali kujenga madarasa zaidi katika shule hiyo sambamba na kuongezwa kwa idadi ya walimu kama njia mojawapo ya kuboresha mazingira ya masomo kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu