News
Kaunti ya Kilifi yashindwa kutumia milioni 220 ya bajeti yake

Ripoti ya mkaguzi wa bajeti nchini imebaini kwamba kaunti ya Kilifi haijatumia mgao wa bajeti ya shilingi milioni 220 uliotengewa mpango wa kushughulikia athari za mabadiliko ya hewa na tabia nchi katika kaunti ya Kilifi.
Hii ina maana kwamba fedha hizo sasa zitalazimika kurejeshwa kwenye hazina kuu ya taifa kama mojawapo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa baada ya kaunti kushindwa kutumia fedha ilizotengewa.
Kwa mujibu ya ripoti hiyo, hii sio mara ya kwanza kwa kaunti ya Kilifi kushindwa kutumia mgao wa fedha inayotengewa kwani mnamo 2023 kiasi cha fedha kipatacho milioni 30.6 zilizotengewa miradi ya maendeleo kwa maeneo bunge hazikutumika fedha hizo zikalazimika kurejeshwa kwenye serikali kuu.
Msimamizi wa bajeti, Margaret Nyakang’o alihoji kwamba kwa jumla kaunti ya Kilifi ilifeli kutumia nusu ya bajeti iliyotengewa mwaka 2023- 2024 maswali yakiibuka kuwa ni vipi kaunti ya Kilifi inamudu kustawi kupitia raslimali zinazopaswa kumnufaisha mwanachi wa Kilifi.
Taarifa yake Hamisi Kombe
News
Anselim, ashutumu utovu wa usalama Taita Taveta

Kaimu Spika katika bunge la kaunti ya Taita Taveta Anselim Mwadime alieleza kusikitishwa na mauaji ya mhudumu mmoja wa bodaboda aliyeuliwa na kisha pikipiki yake kuchukuliwa katika eneo la chuo kikuu cha Taita Taveta.
Mwadime alisema kuna baadhi ya abiria ambao ni wahuni hubebwa na kisha kuwashambulia wahudumu wa pikipiki hadi kuwaua au hata kutoweka na pikipiki.
Aidha, Mwadime alisema kama viongozi wa kaunti ya Taita Taveta hawataruhusu visa hivyo kuendelezwa katika kaunti hiyo.
Vilevile, Mwadime aliishinikiza idara ya usalama kwenye kaunti ya Taita Taveta kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika sekta ya bodaboda na wanaohusika wakabiliwe kisheria.
“Hili jambo linafaa kufuatiliwa kwa undani. Na tunalilaani vikali sisi kama viongozi wa Taita Taveta’’ alisema Mwadime.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Viongozi wahimizwa kushirikiana kubuni ajira kwa vijana

Mwakilishi wa wadi ya Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rose Baraka alitoa wito kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na wawekezaji katika kaunti ya Kilifi ili kudhibiti changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Rose alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye utumizi wa mihadarati sawa na uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa shirika la SHOFCO pamoja na wakaazi wa Sabaki, Rose aliahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii katika juhudi za kuwasadia wananchi kujiendeleza kupitia mpango wa ajira.
“Vijana ni wengi, kazi ni kidogo. Sisi kama viongozi tunastahili kutia bidii kutafuta haya mashirika ili tuangalie vijana wetu wasaidika vipi’’ alisema Rose Baraka.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la SHOFCO eneo la Magarini Kelvin Mtawali Karisa aliupongeza ushirikiano wa mwakilishi wa wadi huyo na shirika hilo na kuwataka vijana kujiunga kwenye makundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo ya kujiendeleza kimaisha.
Taarifa ya Janet Mumbi