News
Usalama na Elimu zavuna kwenye bajeti ya kitaifa

Waziri wa Fedha nchini John Mbadi alisoma bajeti ya kitaifa ya mwaka wa Fedha wa 2025/2026 ambayo ni makadirio ya takriban shilingi trilioni 4.23.
Akisoma bajeti hiyo katika majengo ya bunge la kitaifa, Waziri Mbadi alisema mgao wa shilingi trilioni 3.13 ni matumizi ya kawaida ya serikali, shilingi bilioni 693.2 kwa matumizi ya maendeleo na mgao wa shilingi bilioni 474.9 ukitengewa serikali za kaunti.
Katika bajeti hiyo, Waziri Mbadi alipendekeza mgao wa shilingi bilioni 202 kwa idara ya ulinzi nchini, shilingi bilioni 125.7 kwa huduma ya usalama wa kitaifa, shilingi bilioni 51.4 zikitengwa idara ya ujasusi nchini, shilingi bilioni 32.5 kwa idara ya polisi nchini na shilingi bilioni 38.1 kwa idara ya magereza.
Waziri Mbadi alipendekeza mgao wa shilingi bilioni 138.1 kwa sekta ya Afya ili kufanikisha miradi mbalimbali ikiwemo ule wa Afya kwa wote UHC, shilingi bilioni 3.8 kwa masuala ya ardhi nchini huku shilingi bilioni 82.8 kwa sekta ya Kilimo nchini.

Waziri Mbadi, na wabunge katika majengo ya bunge la kitaifa.
Hata hivyo sekta ya elimu nchini ilitengewa mgao wa shilingi bilioni 702.7, ambapo shilingi bilioni 387.2 zimetengwa kuajiri walimu wa CBC, shilingi bilioni 5.9 kusimimia mitihani ya kitaifa, shilingi bilioni 7 kusimamia masomo ya shule za msingi, shilingi bilioni 51.9 kusimamia shule za upili na shilingi bilioni 28.9 kwa sekondari msingi.
Kulingana na Waziri Mbadi, Serikali imepunguza ushuru wa mchele kutoka nje, Wajenzi na wanaofanya kazi za ngozi wamepata afueni huku Mbadi akiongeza ushuru wa bidhaa za Anasa kama vileo Wageni wanaofanya biashara za pesa mtandaoni kulipia
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Familia ya jamaa aliyezama baharini inalilia haki

Familia ya Mwanamme aliyezama baharini katika kaunti ya Kilifi siku kadhaa zilizopita, inahimiza serikali kuongeza juhudi na kuwapa msaada wa kumtafuta jamaa wao.
Ikiongozwa na Omar Ali Omar ambaye ni Kakake Marehemu, Familia hiyo ilisema wamekuwa na wakati mgumu wa kuelekea baharini kila siku kwani kufikia sasa ni siku ya nne tangu jamaa wao azame baharini.
Aidha aliitaka serikali ya kaunti kutoa taarifa sehemu mbalimbali zinazopakana na ufuo wa bahari kwani huenda mwili wa Marehemu ukasukumwa na mawimbi hadi ufuoni.

Familia ya jamaa aliyezama maji inalilia haki
Omar aliitaka idara ya kukabiliana na majanga katika kaunti kushirikiana na wavuvi wengine eneo la Mnarani pamoja na kutuma maboti zaidi kwa ajili ya uokozi wa mwili wa jamaa huyo kwani wamelazimika kugharamikia mafuta ya boti za ziada.
“Rescu timu ni boti moja, hiyo pekee yake kutafuta mtu kwa bahari ni vigumu vyombo vinatakikana vitoke vingi,washirikiene na sisi familia tuwekuongeza vyombo vya baharini kutafuta jamaa wetu, kwa sasa tunagharimika sasa boti kwenda baharini asubuhi na jioni inatugharimu shilingi elfu 16 kwa siku”, alisema Omar.
Kauli ya Omar imeungwa mkono na Mamake Marehemu ambaye ameshinikiza serikali ya kaunti kuingilia kati na kuhakikisha mwili wa mwanawe unapatikana.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Nassir: Kaunti ya Mombasa wametenga milioni 80 za Afya

Gavana wa kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir amesema serikali ya kaunti ya Mombasa wametenga shilingi milioni 80 kugharamia sehemu ya matibabu ya wakaazi ambao hutibiwa katika hospitali za Level 4 na Level 5.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Nassir alisema fedha hizo zitagharamia bima ya afya ya SHA ya wenyeji wa kaunti hiyo kwa muda wa mwaka mmoja.
Gavana Nassir pia alisema fedha hizo zitagharamia madeni ya ziada ya matibabu kwa watoto wa chini ya umri wa miaka 5 ambao wanatibiwa kupitia bima hiyo ya SHA.
“Tumeweka dawati maalum na fedha kuweza kuwalipia ile amana ambayo ilikuwa inalipiwa SHA. Na itakuwa sio ya Public health pekee lakini kando na Public health mnakuwa mumelipiwa kwa mwaka mzima’’, alisema gavana Nassir
Wakati huo huo Gavana Nassir alieleza matumaini kwamba mpango huo utasaidia kwa asilimia kubwa kuimarisha huduma za matibabu kwa wenyeji wa kaunti hiyo.
Taarifa ya Janet Mumbi