News
Auma: Serikali inahusika na visa vya utekaji nyara

Afisa wa masuala ya dharura katika Shirika la kutetea haki za kibinadamu la MUHURI Francis Auma alisema serikali kuu inahusika na visa vya utekaji nyara licha ya kujitenga na tetesi hizo.
Auma alidai kwamba serikali kuu inahusika kwa asilimia kubwa katika ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini Kenya na inapaswa kuweka wazi suala hilo ili Wananchi wafahamu mahali walipo jamaa zao.
Kulingana na Auma, visa hivyo ambavyo hadi sasa vinaendelea kutekelezwa nchini Kenya vinatekelezwa na serikali kuu.
“Kwa muda mrefu sisi tumepigania masuala haya, watu washikwe, tunataka uwajibikaji na tunataka polisi wawajibike’’, alisema Auma.
Auma pia alipuuzilia mbali msamaha wa Rais William Ruto kwa vijana wa kizazi cha Gen–Z akidai haukuwa wa kweli na ulilenga kuwafumba macho wakenya hasa familia ambazo ziliwapoteza wapendwa wao wakati wa maadamano ya Gen -Z.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Chrispus aomba msahama bunge la kaunti ya Taita Taveta

Mwakilishi wadi ya Bomani mjini Taveta kaunti ya Taita Taveta Chrispus Tondoo ameliomba bunge la kaunti hiyo msamaha kutokana na matamshi aliyoyatoa hapo awali akikashifu bunge hilo kwa madai ya kushamiri kwa visa vya ufisadi na utepetevu.
Tondoo akiomba msamaha katika bunge hilo alisema alitambua athari zilizosababishwa na matamshi hayo kwa wenyeji wa kaunti hiyo na bunge hilo, hali ambayo imemfanya kuchukua hatua hiyo ya kuomba msamaha.
Aidha Tondoo aliahidi kuliheshimu bunge hilo kwa mujibu wa kanuni na Sheria za bunge la kaunti ya Taita Taveta.
‘’Naomba msamaha kutokana na matamshi ambayo niliyatoa tarehe 2 na tarehe 3 mwezi wa Juni mwaka huu wa 2025 kwani hayakuwa yenye heshima kwa wenyeji wa Taita Taveta na bunge la kaunti’’, alisema Tondoo.
Tondoo alikuwa Mwakikishi wa wadi wa pili kuomba msamaha baada ya Mwakilishi wa wadi ya Kaloleni mjini Voi Ahmed Azari kuchukua hatua hiyo mwezi mmoja uliyopita.
Haya yalijiri baada ya kaimu spika wa bunge hilo Anselim Mwadime kuapa kuwachulia hatua za kisheria wanachama wanne wa bunge hilo, wawili wakiwa ni Tondoo na Azari ambayo tayari wameomba msamaha huku wawili wakiwa wamesalia bila kuomba msamaha.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mawakili Kilifi waungana kushtumu mauaji ya Wakili Mbobu

Siku chache baada ya Wakili Kyalo Mbobu kuuawa kinyama kwa kupigwa risasi mara kadhaa akiwa kwenye gari lake barabara ya Lang’ata jijini Nairobi, mawakili mjini Kilifi kaunti ya Kilifi wameungana na mawakili wengine nchini siku ya Ijumaa Semtemba 12 mwaka huu kufanya matembezi ya amani, wakishutumu vikali mauaji hayo.
Wakiongozwa na Mwakilishi wao Sesil Mila, mawakili hao walilaani vikali mauaji ya wakili Mbobu wakiishutumu serikali kwa kutowajibikia swala la usalama wa wananchi wake.
Aidha waliitaka idara ya usalama kuhakikisha kuwa inafanikisha wajibu wake wa kuwalinda mawakili wakisisitiza haja ya haki kupatikana kwa familia ya mwendazake wakili Kyalo.

Mawakili wa Kilifi wakiongozwa na Sesil Mila, washtumu mauaji ya Wakili Kyalo Mbobu
Mawakili hao sasa waliitaka idara ya upelezi na asasi zote husika kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina unafanywa kubaini watuhumiwa wa mauaji hayo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria haraka iwezekanavyo.
Taarifa ya Hamis Kombe