Business
Ali Mbogo Aitaka Pwani Kuwawezesha Vijana Kunufaika na Uchumi wa Baharini

Serikali za kaunti za pwani zimetakiwa kuwawezesha vijana katika masuala ya ubaharia ili kujiendeleza kiuchumi.
Aliyekuwa mbunge wa Kisauni, Ali Mbogo, amesema kuwa ukosefu wa mikakati mwafaka kutoka kwa viongozi kuwawezesha vijana umechangia vijana wengi kukosa vibali muhimu vinavyohitajika ili kuajiriwa katika sekta hiyo ya uchumi wa baharini.
Mbogo ameeleza kuwa Pwani iko na fursa nyingi za kiuchumi kupitia bahari, na ni jambo la kusikitisha kuona vijana wakiachwa nyuma kwa kukosa mafunzo na vyeti vinavyotambulika kimataifa ili kuwawezesha kunufaika na ajira hizo.
Wakati uo huo mwenyekiti huyo wa bodi ya bandari ya LAPSSET amewahimiza vijana ambao hawakubahatika kuendelea na masomo, kujiunga na vyuo vya ufundi ili wapate ujuzi wa kazi za mkono na vyeti vitakavyowawezesha kupata ajira.
“Kuna nafasi nyingi sana katika bandari ya Mombasa lakini tuliowachangua hawatujali bali kujijali wenyewe.”
Business
Bei ya vitunguu katika masoko ya humu nchini kuongezeka

Bei ya Vitunguu katika masoko ya humu nchini huenda ikaongezeka hata zaidi kufuatia uhaba wa bidhaa hiyo.
Kufuatia hatua hiyo wafanyibiashara wa vitunguu humu nchini wamelazimika kuagiza bidhaa hiyo kutoka taifa jirani la Tanzania kufuatia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.
Wakizungumza na vyombo vya habari, Wafanyibiashara hao walisema kuna uhaba mkubwa wa vitunguu jambo ambalo limefanya bei kupanda.
Kulingana na wakulima wa zao hilo, hawakupanda vitunguu kutakana na gharama ya juu ya mbegu pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya anga.
Aidha walisema kuwa gharama ya Kilimo cha vitunguu imekuwa juu ikilinganishwa na mapato ya chini na ukosefu wa bei nzuri sokoni.
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
KEMFRI kuanzisha mradi maalum wa kuzalisha mbegu za samaki

Taasisi ya utafiti wa bahari na uvuvi nchini, KEMFRI, imeanzisha mradi maalum wa kuzalisha mbegu za samaki, ili kuongeza upatikanaji wao na kuinua sekta ya uvuvi nchini.
Akizungumza jijini Mombasa, kaimu mkurugenzi mkuu wa KEMFRI, Dkt. James Mwaluma, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa katika eneo la Shimoni kaunti ya Kwale na unalenga kuzalisha samaki wa thamani kubwa kama vile kamba, matiko, na aina nyingine ambazo upatikanaji wake ni nadra.
Dkt. Mwaluma alisema kuwa mbegu zitakazozalishwa kupitia mradi huo zitasambazwa kwa vikundi vya vijana na wanawake wanaojihusisha na shughuli za ufugaji wa samaki, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Aidha, aliwahimiza vijana kote nchini wakumbatie fursa zilizopo kwenye uchumi wa baharini akisema ni njia mojawapo ya kujikwamua kimaisha na kupambana na ukosefu wa ajira.
Taarifa ya Pauline Mwango