Sports
Harambee Stars Wapiga Ushelisheli Kasarani, Olunga Asawazisha Rekodi ya Oliech

Timu ya soka Harambee Stars hatimaye wamehitimisha kusubiri ushindi wa nyumbani kwenye kufuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya kushinda kwa kishindo cha mabao 5-0 dhidi ya UShelisheli katika uwanja uliojaa mashabiki wa Kasarani Jumanne alasiri.
Kocha mkuu Benni McCarthy alifanya mabadiliko sita kutoka kwa kikosi kilichopoteza 3-1 dhidi ya Gambia wiki iliyopita. Kipa Brian Bwire alimchukua nafasi Byrne Omondi langoni, huku Ronney Onyango akibaki beki wa kulia.
Kwa kuwa Aboud Omar alikuwa amesimamishwa, Manzur Okwaro alicheza katika nafasi yake ya asili kama beki wa kushoto mabadiliko yaliyokaribishwa baada ya kuonesha uwezo mkubwa katika michuano ya CHAN 2024 kama kiungo mkabaji. Kwenye moyo wa safu ya ulinzi, Sylvester “Sili” Owino na Collins Shichenje waliendeleza ushirikiano wao, wakilindwa na Alpha Chris Onyango, aliyemchukua nafasi Richard Odada. Aliungana na Duke Abuya katikati ya uwanja, huku Ryan-Wesley Ogam akichukua nafasi ya Timothy Ouma Noor, akicheza kama namba tisa ya uongo.
Job Ochieng’, aliyeng’aa alipoingia kama mchezaji wa akiba dhidi ya Gambia, alianza kwenye wingi wa kushoto mbele ya Emmanuel Osoro, huku Wilson Lenkupae anayekipiga Australia akicheza wingi wa kulia. Nahodha Michael Olunga aliongoza safu ya mashambulizi.
Mashabiki hawakungojea kwa muda mrefu. Dakika ya 7, nyota wa moto Ogam alivunja kimya kwa kumalizia kwa ustadi.
Kenya walimiliki mpira na kuongeza bao la pili dakika ya 35 kupitia Collins Shichenje aliyemalizia pasi ya Abuya. Dakika tatu baadaye, Ogam alifunga tena — bao lake la nne katika mechi sita pekee — na kufanya matokeo kuwa 3-0. Kabla ya mapumziko, Olunga alifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya Ogam kuangushwa ndani ya kisanduku, na kuwapa Stars uongozi wa 4-0 kipindi cha kwanza.
Bao hilo lilimfanya Olunga kufikia rekodi ya Dennis Oliech ya mabao 34, na kumfanya awe mfungaji wa pili bora wa muda wote wa Kenya kwa pamoja.
Kipindi cha pili, McCarthy aliwatoa Ochieng’, Lenkupae na Abuya na kuwaingiza Ben-Stanley Omondi, Boniface Muchiri na Marvin Nabwire. Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya 68, Olunga aliporuka juu na kufunga kwa kichwa kutoka krosi safi ya Onyango, na kuhitimisha ushindi wa 5-0.
Licha ya Kenya kutokuwa na nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, Kanada na Mexico, ushindi huu uliwaweka katika nafasi ya nne Kundi F wakiwa na pointi 9 — moja nyuma ya Burundi na mbili juu ya Gambia, waliotarajiwa kukutana usiku huo. Stars sasa wanageuza macho yao kwenye mechi za mwisho za kufuzu mwezi Oktoba, ambapo watakutana na Burundi (Okt 6) na vinara wa kundi Ivory Coast (Okt 13).
Ivory Coast kwa sasa wanaongoza kundi wakiwa na pointi 19, wakiwa pointi moja mbele ya Gabon walioko nafasi ya pili.
Sports
Uingereza yawapa wapinzani onyo baada ya kuichapa Serbia 5-0, Haaland apiga mabao matano kwa Norway

Timu ya taifa la Uingereza ilituma onyo kali kwa wapinzani wao wa Kombe la Dunia baada ya kuifumua Serbia 5-0 katika mchezo wa kufuzu siku ya Jumanne, huku Erling Haaland akifunga mabao matano na kuisaidia Norway kuendeleza rekodi ya ushindi wa asilimia 100.
Kwingineko barani Ulaya, Ureno na Ufaransa ziligeuza matokeo baada ya kuwa nyuma na kupata ushindi wa pili mfululizo katika harakati zao za kufuzu kwa michuano ya mwakani itakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Ubora wa kikosi cha Thomas Tuchel ulitiwa shaka baada ya ushindi hafifu wa 2-0 dhidi ya Andorra siku ya Jumamosi huko Villa Park, lakini safari hii walitoa jibu tosha.
Uingereza ilidhibiti dakika za mwanzo mjini Belgrade na kufungua ubao dakika ya 33, wakati Harry Kane alipofunga bao lake la 74 la kimataifa kwa kichwa akimalizia kona ya Declan Rice. Wageni waliongeza bao dakika mbili baadaye, Noni Madueke akimalizia pasi nzuri ya kichwa kutoka Morgan Rogers na kumchambua kipa wa Serbia, Djordje Petrovic.
Bao la tatu lilipatikana dakika ya 52, Ezri Konsa akipiga shuti kufuatia mpira uliorudi baada ya adhabu ndogo na kufunga bao lake la kwanza la kimataifa.
Mpira mwingine wa adhabu uliopigwa na Rice ulipelekea bao la nne, Marc Guehi akiteleza na kufunga kufuatia faulo iliyofanywa dhidi ya Kane na Nikola Milenkovic, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu moja kwa moja.
Mbadala Marcus Rashford alifunga kwa mkwaju wa penalti mwishoni na kukamilisha usiku bora kwa Uingereza.
Uingereza sasa inaweza kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya nane mfululizo kwenye mchezo wao ujao wa Kundi K dhidi ya Latvia mwezi ujao.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Albania ilipanda hadi nafasi ya pili baada ya kuishinda Latvia 1-0 jijini Tirana.
Sports
Sare Tasa na Burkina Faso Yaahirisha Ndoto za Misri Kufuzu Kombe la Dunia

Matumaini ya taifa la Misri la kufuzu Kombe la Duniabado baada ya kutoka sare tasa ya 0-0 dhidi ya Burkina Faso kwenye mechi ya Kundi A iliyochezwa Ouagadougou, Jumanne.
Kikosi cha Hossam Hassan ambacho hakijapoteza mchezo wowote kimefikisha pointi 20 na kuongoza Kundi A kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Burkina Faso, huku kukiwa na mechi mbili pekee zikisalia kwenye mchujo.
Kwa kuwa ni washindi wa makundi pekee wanaofuzu moja kwa moja, mabingwa wa Afrika mara saba wanahitaji alama mbili pekee kutoka kwa michezo yao miwili ya mwisho ili kujihakikishia nafasi na kufanikisha ushiriki wao wa nne kwenye Kombe la Dunia. Watakutana na Djibouti na Guinea-Bissau mwezi Oktoba.
Kocha wa Misri, Hassan, hata hivyo, alisherehekea matokeo hayo ambayo yamewasogeza hatua moja karibu na kufuzu katika mashindano makubwa ya timu 48 yatakayofanyika Amerika Kaskazini mwaka ujao.
“Ni siku kubwa kwa watu wa Misri… Ningependa kuwashukuru kila mchezaji kwa juhudi zao dhidi ya timu ngumu ambayo ina wachezaji wanaocheza Premier League, Bundesliga na Ligue 1,” alisema Hassan, mshambuliaji wa zamani wa Misri aliyewaongoza kufuzu Kombe la Dunia mwaka 1990, akizungumza na kituo cha On Sport.
“Licha ya kucheza ugenini Burkina Faso, tulicheza kwa mtindo chanya na kuunda nafasi kubwa. Wakati huohuo, tulidumisha uwiano. Tungelikuwa tumefunga goli moja au mawili kabla ya mwisho,” aliongeza.
Misri ilipata pigo mapema baada ya mshambuliaji wa Manchester City, Omar Marmoush, kulazimika kutoka nje kwa majeraha dakika ya 9.
Fursa yao bora ilikuja dakika ya 67 wakati Mohamed Salah alipompasia Osama Faisal lakini shuti lake likakataliwa kwa kuotea. Trezeguet wa Misri alikosa nafasi ya kwanza ya mchezo baada ya jaribio lake kuokolewa na kipa wa Burkina Faso, Herve Koffi.
Wenyeji hawakuwa na mashambulizi mengi, huku mshambuliaji wa Sunderland, Bertrand Traore, akiongoza juhudi zao bora.
Misri walikaribia kufunga goli la ushindi dakika za mwisho, lakini Mostafa Mohamed alipoteza nafasi mbili muhimu.
Hassan, ambaye ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Misri, anatarajiwa kuwa wa kwanza kuongoza taifa hilo kufika Kombe la Dunia akiwa mchezaji na pia kocha.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 alisema: “Lengo langu lilikuwa kufundisha timu ya taifa ya Misri. Nimekuwa nikiota kila mara jambo hilo. Nataka kutimiza ndoto ya mashabiki na kuishi kwa imani yao (kwa kuongoza timu kufuzu Kombe la Dunia).”