News
Oyuu: Fedha za Shule Zisambazwe kwa Wakati

Katibu mkuu wa Chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini (KNUT) Collins Oyuu ameitaka serikali kuu kuharakisha mchakato wa kusambaza fedha za kufadhili masomo shuleni.
Oyuu amesema mtaala mpya wa elimu nchini CBC utafaulu iwapo shule zitapokea fedha hizo kwa wakati na ziwe za kutosha.
Katibu huyo amedokeza kwamba walimu wakuu katika shule hizo wanapitia wakati mgumu kuendesha shughuli za shule baada ya serikali kujikokota katika usambazaji wa hela shuleni.
Wakati huo huo amesema baadhi ya walimu wakuu wamekuwa wakijikuta na matatizo ya afya ya akili kutokana na changamoto hizo.
News
Kimotho: Deni lililosalia kwa waathiriwa wa bwawa la Mwache ni shilingi bilioni 2

Serikali imesema itakamilisha malipo ya fidia kwa waathiriwa wote wa ujenzi wa mradi wa Bwawa la Mwache katika eneo la Kinango kaunti ya Kwale ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Katibu katika Idara ya unyunyizaji maji nchini Ephastus Kimotho amesema deni lililosalia kwa waathiriwa wa mradi huo ni shilingi bilioni 2 na tayari limeanza kulipwa.
Kimotho amesema hatua hiyo imeafikiwa baada ya Tume ya kitaifa ya ardhi NLC kupewa shilingi milioni 600 ambazo zitapewa waathiriwa kama fidia kuanzia wiki ijayo.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo sawa na kuzindua kituo cha afya cha Mazeras kinachojengwa kama sehemu ya mradi huo, Kimotho amesema fedha zilizosalia zitaanza kutolewa kuanzia mwezi Julai ili kuafikia mipango iliyowekwa.
“Kufikia mwezi Julai mwaka huu tutakuwa tumeanza kusambaza mgao mwengine wa fedha zilizosalia ili kukamilisha fidia hizo kufikia mwezi Disemba mwaka huu”, alisema Kimotho.
Shughuli za ujenzi wa Bwawa la Mwache
Kwa upande wake Gavana wa Kwale Fatuma Achani amesema mradi huo uko na manufaa mengi kwa wakaazi wa kaunti ya Kwale ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, miongoni mwa manufaa mengine.
“Tumeona manufaa mengi kupitia mradi huu, umeleta vituo vya afya karibu na wananchi, ujenzi wa shule za Chekechea na miradi mingi muhimu ya umma, hivyo basi tunafaa kuunga mkono kikamilifu”, alisema Gavana Achani.
Mradi huo ambao ulikuwa umetengewa shilingi bilioni 4.6 kama fidia ya wakaazi waliopeyana ardhi zao kwa ujenzi wa mradi huo zimekuwa zilipiwa kwa njia ya awamu hali ambayo ilisababisha maandamano kutokana na kucheleweshwa kwa fidia hiyo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Watu watatu wakamatwa katika Mahakama ya Milimani

Watu watatu wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wa kaunti ya Trans Nzoia wamekamatwa na maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia sare baada ya kusikiza kesi inayomkabili gavana wa kaunti hiyo George Natembeya katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi.
Watatu hao walikamtwa mda mfupi baada ya Jaji Zipporah Gichana, kuagiza upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi dhidi ya kesi ya ufisadi inayomkabili gavana huyo.
Agizo hilo lilifuata tamko la upande wa mashtaka kwamba ilifeli kufuta agizo la awali la Mahakama la kuwasilisha ushahidi.
“Nyaraka na taarifa hizo zilipaswa kuwa zimetolewa kufikia sasa, kwa hiyo ninaelekeza upande wa mashtaka kufuata maagizo ya awali”, aliagiza Jaji Gichana.
Upande wa mashtaka uliomba mda wa wiki mbili zaidi ili kutii maagizo ya awali ya kuwasilisha ushahidi wa nyaraka.
“Hati nyingi zinapatikana kutoka kaunti ya Trans Nzoia na tumeshindwa kuzipata, tunaomba wiki mbili za ziada ili kutii,” Wakili wa Serikali Victor Awiti aliwasilisha.
Hata hivyo, upande wa utetezi ulipinga ombi hilo, ukisema ni sawa na matumizi mabaya ya mchakato wa Mahakama.
Upande wa mashtaka uliamriwa kufichua nyenzo zote husika kabla ya Juni 16 kesi hiyo itakapotajwa.
Taarifa ya Joseph Jira