News
Ruku: Serikali kuajiri vijana laki moja kwa NYS

Serikali inalenga kuajiri zaidi ya vijana laki moja katika Shirika la huduma kwa vijana wa taifa NYS.
Waziri wa utumishi wa umma nchini Geoffrey Ruku amesema hatua hiyo itachangia kuboreshwa kwa huduma za umma sawa na kuhakikisha Shirika la NYS linakuwa nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika kaunti ya Machakos, Waziri Ruku amesema hatua hiyo itapunguza utegemeaji wa ufadhili wa umma kwani shirika hilo itapanua mikakati bora ya serikali ya kibiashara pamoja na kufanikisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Ruku amelishinikiza bunge la kitaifa kuharakisha marekebisho ya mswada wa NYS ambao utawalishwa na Wizara yake bungeni ili kusawazisha mfumo wa kisheria wa shirika hilo.
Wakati huo huo amewataka vijana kukumbatia mipango ya serikali ya kujumuisha wananchi wote pamoja katika kufanikisha ajenda ya serikali ya maendeleo endelevu hadi mashinani.
News
Nyakang’o, apendekeza mgao wa shilingi bilioni 1.6

Mdhibiti wa bajeti nchin Margaret Nyakang’o amependekeza kuongezwa kwa kiwango cha bajeti ya ofisi yake kutoka shilingi milioni 7.2 hadi shilingi bilioni 1.6 ili kufanikisha majukumu yake.
Akizunguza mjini Mombasa wakati wa kikao na kamati ya uekezaji wa umma na hazina maalum katika bunge la Seneti, Nyakang’o amesema bajeti hiyo ya ofisi yake iko chini mno katika kufanikisha mikakati endelevu ya majukumu yake ya kikazi.
Hata hivyo amesema iwapo bajeti hiyo itaongezwa ofisi yake itakuwa na wakati mwafaka wa kukagua miradi ya maendeleo katika kaunti zote nchini.
News
Gavana Mung’aro afanya kikao na Gach Group kuhusu uekezaji wa Madini

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro amefanya kikao cha mazungumzo na waekezaji kutoka Kampuni ya Gach Group kuhusu uekezaji wa madini katika eneo la Magarini utakavyochangia pato la kaunti.
Kulingana na Gavana Mung’aro, uwekezaji huo utafungua nafasi za ajira kwa zaidi ya watu 500 wa eneo bunge la Magarini na kaunti ya Kilifi kwa jumla kwani waekezaji hao wanalenga madini ya Titanium na lime.
Gavana Mung’aro ameweka wazi kwamba serikali yake imejitolea kuweka mazingira bora kwa waekezaji sawa na kufanikisha mpango endelevu wa kibiashara utakaowanufaisha wenyeji.
Akizungumza baada ya kukutana na waekezaji hao kutoka taifa la Gambia, Gavana Mung’aro amedokeza kwamba kaunti ya Kilifi iko tayari kushirikiana na waekezaji wenye malengo bora kwa wananchi ili kufanikisha maendeleo.
Hata hivyo viongozi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mwenyekiti wa Gach Group Dkt Abubakar Jawara, aliyekuwa Mbunge wa Magarini Harrison Kombe, aliyekuwa Seneta wa Samburu Sammy Leshore pamoja na viongozi wengine wa kaunti.