News
Mwinyi: Serikali izuie Ubomozi wa Nyumba Elfu moja Changamwe

Viongozi wa kisiasa kaunti ya Mombasa wanaitaka serikali kuingilia kati na kuzuia ubomozi wa nyumba zaidi ya elfu moja katika maeneo ya Chaani, Migadini, Lilongwe na Portreitz katika eneo bunge la Changamwe.
Wakiongozwa na Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi, viongozi hao wamesema baadhi ya wanasiasa walio uongozini wamekuwa wakisaidia mabwenyenye kunyakua ardhi za wananchi walalahoi.
Akizungumza na Wanahabari katika eneo bunge lake, Mwinyi ameitaka serikali kutafuta suluhu la kudumu la migogoro ya mashamba katika kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kwa jumla.
Mbunge huyo hata hivyo amewataka wanasiasa kukoma kuwanyanyasa wananchi na badala yake kuwahudumia bila ubaguzi ili kuzikabili changamoto mbalimbali mashinani.
Kauli yake imejiri baada ya familia nyingi katika maeneo ya Chaani, Migadini, Lilongwe na Portreitrz kulalamikia ubomozi wa nyumba zao bila mikakati mwafaka ya kuhamishiwa katika ardhi mbadala.
News
Nyakang’o, apendekeza mgao wa shilingi bilioni 1.6

Mdhibiti wa bajeti nchin Margaret Nyakang’o amependekeza kuongezwa kwa kiwango cha bajeti ya ofisi yake kutoka shilingi milioni 7.2 hadi shilingi bilioni 1.6 ili kufanikisha majukumu yake.
Akizunguza mjini Mombasa wakati wa kikao na kamati ya uekezaji wa umma na hazina maalum katika bunge la Seneti, Nyakang’o amesema bajeti hiyo ya ofisi yake iko chini mno katika kufanikisha mikakati endelevu ya majukumu yake ya kikazi.
Hata hivyo amesema iwapo bajeti hiyo itaongezwa ofisi yake itakuwa na wakati mwafaka wa kukagua miradi ya maendeleo katika kaunti zote nchini.
News
Gavana Mung’aro afanya kikao na Gach Group kuhusu uekezaji wa Madini

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro amefanya kikao cha mazungumzo na waekezaji kutoka Kampuni ya Gach Group kuhusu uekezaji wa madini katika eneo la Magarini utakavyochangia pato la kaunti.
Kulingana na Gavana Mung’aro, uwekezaji huo utafungua nafasi za ajira kwa zaidi ya watu 500 wa eneo bunge la Magarini na kaunti ya Kilifi kwa jumla kwani waekezaji hao wanalenga madini ya Titanium na lime.
Gavana Mung’aro ameweka wazi kwamba serikali yake imejitolea kuweka mazingira bora kwa waekezaji sawa na kufanikisha mpango endelevu wa kibiashara utakaowanufaisha wenyeji.
Akizungumza baada ya kukutana na waekezaji hao kutoka taifa la Gambia, Gavana Mung’aro amedokeza kwamba kaunti ya Kilifi iko tayari kushirikiana na waekezaji wenye malengo bora kwa wananchi ili kufanikisha maendeleo.
Hata hivyo viongozi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mwenyekiti wa Gach Group Dkt Abubakar Jawara, aliyekuwa Mbunge wa Magarini Harrison Kombe, aliyekuwa Seneta wa Samburu Sammy Leshore pamoja na viongozi wengine wa kaunti.