Waendeshaji mashtaka nchini Morocco Alhamisi waliomba mahakama kuwahukumu kifungo cha hadi miaka miwili jela mashabiki 18 wa soka kutoka Senegal walioko rumande mjini Rabat tangu fainali ya AFCON ya mwezi uliopita, wakituhumiwa kwa “uhuni wa michezo”, mwanahabari wa AFP ameripoti.
Upande wa mashtaka uliomba adhabu ya juu zaidi kwa baadhi ya washtakiwa, ukidai kuwa walikusudia kwa makusudi kuvuruga mwenendo wa kawaida wa mechi hiyo.
Mashtaka yalieleza kuwa kundi hilo “lilifanya vitendo vya vurugu vilivyorushwa moja kwa moja kwenye televisheni,” huku washtakiwa wakikana tuhuma zote dhidi yao.
Mashabiki hao wa Senegal wamekuwa rumande tangu Januari 18, siku ya fainali ya AFCON iliyokuwa na ushindani mkali ambapo Morocco walifungwa 1-0 na Senegal wakiwa nyumbani.
Dakika chache kabla ya kumalizika kwa mechi, baadhi ya mashabiki wa Senegal walijaribu kuingia uwanjani, huku wachezaji wa Senegal wakisimamisha mchezo kwa takriban dakika 20 kupinga penalti ya dakika za mwisho iliyotolewa kwa Morocco.
Baadhi ya mashabiki pia walionekana wakirusha vitu uwanjani, ikiwemo kiti.
Upande wa mashtaka ulisema ushahidi dhidi ya washtakiwa unatokana na picha za kamera za ulinzi zilizowekwa uwanjani, pamoja na ripoti za kitabibu zinazoonyesha majeraha kwa maafisa wa usalama na wasimamizi wa uwanja.
Aidha, uharibifu wa miundombinu ya uwanja unakadiriwa kufikia zaidi ya dirham milioni 4 za Morocco (takriban dola 430,000), kwa mujibu wa mashtaka.
