Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Michezo na Utamaduni Alhamisi imekataa pendekezo la Wizara ya Michezo la kuongeza bajeti ya maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Haya yanajiri huku ikibainika kuwa Kenya bado haijalipa ada ya lazima ya Shilingi bilioni 3.5 ili kuthibitisha nafasi yake kama mwenyeji wa mashindano hayo ya bara Afrika.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Webuye Magharibi, Dan Wanyama, ilitupilia mbali ombi la wizara la kuongeza bajeti ya maandalizi kutoka Shilingi bilioni 3.5 hadi Shilingi bilioni 5, ikisema hoja zilizotolewa hazitoshi kuhalalisha nyongeza hiyo.
“Badala yake, mnapaswa kupunguza bajeti kwa sababu mashindano haya yanaandaliwa na nchi tatu. Msukumo wa kuongeza fedha haupaswi kulinganishwa na nchi iliyoandaa AFCON peke yake,” alisema Wanyama.
Msimamo huo mkali ulijiri baada ya Katibu Mkuu wa Michezo, Elijah Mwangi, kufichua kuwa Kenya bado haijawasilisha Shilingi bilioni 3.5 zinazohitajika na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kutokana na ukosefu wa fedha.
Kenya imepangwa kuandaa AFCON 2027 kwa pamoja na Uganda na Tanzania kupitia zabuni ya pamoja ya “Pamoja Bid”. Kwa mujibu wa PS huyo, Uganda na Tanzania tayari wamelipa ada inayotakiwa na CAF ili kuthibitisha uenyeji wao.
“Wenzetu Uganda na Tanzania tayari wametimiza wajibu wao kwa kulipa ada inayohitajika,” Mwangi aliambia kamati wakati wa majadiliano kuhusu Taarifa ya Sera ya Bajeti ya mwaka 2026.
Wizara ya Michezo ilikuwa imeomba kamati kuingilia kati ili fedha hizo zijumuishwe katika bajeti ya nyongeza, ili Kenya iweze kutimiza wajibu wake na kuepuka kuhatarisha hadhi yake mbele ya CAF.
Akijitetea kuhusu pendekezo la kuongeza bajeti, Mwangi alisema aliongoza ujumbe uliowahusisha maafisa wa soka nchini katika ziara ya kujifunza nchini Morocco wakati wa AFCON iliyopita.
“Tulibaini kuwa ili kufikia viwango vilivyowekwa Morocco, ni lazima tuongeze bajeti,” alisema.
Hata hivyo, wabunge walisisitiza kuwa mchango wa kifedha wa Kenya unapaswa kuzingatia ukweli kwamba ni mwenyeji mwenza na nchi mbili nyingine, hali inayopaswa kupunguza mzigo wa kifedha.
Licha ya kukataa nyongeza ya bajeti, kamati ilihakikishia wizara kuwa itaunga mkono juhudi za kushirikiana na Hazina ya Kitaifa ili fedha za ada ya uenyeji zitolewe kwa wakati.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Sera ya Bajeti, kiwango kilichopendekezwa kwa Idara ya Michezo katika mwaka wa kifedha 2026/27 ni Shilingi bilioni 25.49, zikiwemo Shilingi bilioni 7.38 za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 18.11 za maendeleo.
