Mshtakwa wa kesi ya Shakahola alikiri makosa 43 ya mauaji

Mshtakwa wa kesi ya Shakahola alikiri makosa 43 ya mauaji

Kesi ya mauaji bila kukusudia inayomhusisha Mhubiri tata Paul Mackenzie na wenzake imechukua mkondo mpya baada ya mmoja wa washtakiwa kuingia katika makubaliano ya kukiri makosa na upande wa mashtaka.

Mshtakiwa huyo Enos Amanya Ngala, anayejulikana kama “Hallelujah” na ambaye alikuwa akikabiliwa na mashtaka pamoja na Paul Mackenzie, alikiri makosa 43 ya mauaji bila kukusudia baada ya kushtakiwa upya.

Enos alikiri makosa hayo kwa hiari bila kushinikizwa, kutishwa au kulazimishwa.

Kupitia makubaliano, Amanya aliahidi kurekodi taarifa kwa wachunguzi na kutoa ushahidi kama shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi inayoendelea ya Shakahola, pamoja na kesi nyingine zinazohusiana.

Kwa upande wake, Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP ilikubali kuondoa mashtaka 195 kati ya mashtaka 238 ya awali yaliyokuwa yakimkabili, pamoja na kuondoa mashtaka yote yaliyokuwa katika Mahakama ya watoto ya Tononoka.

Upande wa mashtaka uliiomba Mahakama imchukulie Amanya kama mkosaji wa kwanza na kumpa kifungo cha miaka 11 badala ya kifungo cha maisha, kwa kuzingatia kuwa tayari ametumikia miaka mitatu rumande.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa huku zaidi ya mashahidi 100 tayari wakiwa wametoa ushahidi wao.

Taarifa ya Mwanahabari wetu