News
Ethekon: Tutaandaa uchaguzi huru na haki, 2027
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imewahakikishia wakenya kwamba itafanikisha uchaguzi huru na haki ifikapo mwaka wa 2027.
Kulingana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Erastus Ethekon, IEBC iko tayari kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, ikiwemo usajili wa wapiga kura, kuendesha uchaguzi, pamoja na kugawaa mipaka ya maeneo ya uwakilishi.
Akizungumza mjini Mombasa tangu kuapishwa kwake kushikilia wadhfa ya Mwenyekiti wa IEBC, Ethekon alisema IEBC itaharakisha mchakato wa kuandaa chaguzi ndogo 23 kote nchini ikiwemo nafasi moja ya Seneta, nafasi 6 za ubunge na nafasi 16 za uwakilishi wadi.
Ethekon alisema nafasi hizo za viongozi ziliachwa wazi baada ya baadhi ya viongozi kupoteza maisha yao huku wengine viti vya vikasalia wazi baada ya matokeo ya chaguzi hizo kubatilishwa na Mahakama.
Wakati huo huo aliwataka wanasiasa kujiepusha na matamshi yanayoashiria uwepo wa njama za wizi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao, akisema kauli hizo zinatia doa utendakazi wa tume ya IEBC huku akilitaka bunge la kitaifa pamoja na Wizara ya Fedha nchini kuhakikisha tume hiyo inapokea mgao wa fedha kwa wakati.
Ethekon alisisitiza kuwa tume hiyo iko imara na haitashuhudia migawanyiko kama ilivyoshuhudiwa katika vipindi vilivyopita.
Taarifa ya Mwanahabari wetu